Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John
Pombe Magufuli amekutana na kufanya mazungumzo na viongozi wanne Ikulu Jijini
Dar es salaam ambapo pamoja na kutakiana heri ya Mwaka Mpya, wamezungumzia
mambo mbalimbali kuhusu mustakabali wa Serikali ya awamu ya Tano ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania.
Akizungumzia yaliyojiri katika Mazungumzo hayo,
Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Profesa Mussa Juma Assad
amesema wamezungumzia kupunguza gharama za matumizi ya kuendesha serikali na
kuongeza ukusanyaji wa mapato ya Serikali.
Profesa Assad amebainisha kuwa Rais Magufuli
ametaka Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ihakikishe
Tanzania inaongeza ukusanyaji wa mapato kutoka asilimia 14 ya pato la Taifa
(GDP) kwa mujibu wa hesabu zilizofanyika mwaka juzi.
"Hadi Mwaka juzi Tanzania ilikua inakusanya
mapato kwa kiwango cha asilimia 14 ya pato la Taifa ikilinganishwa na Kenya
ambayo ilikua ikikusanya asilimia 19 ya pato Taifa, na hakuna sababu za Msingi
za kwa nini Tanzania iwe nyuma katika ukusanyaji wa mapato hayo" aliongeza
Profesa Assad.
Rais Magufuli pia amekutana na Mkurugenzi wa
Mashitaka hapa Nchini (DPP) Mheshimiwa Biswalo Eutropius Mganga ambaye amesema
mazungumzo yao yalijikita katika suala la kupeana mikakati ya namna ofisi ya
Mkurugenzi wa Mashitaka inavyopaswa kufanya kazi ili kuendana na kauli mbiu ya
serikali ya awamu ya tano isemayo "Hapa Kazi Tu"
Aidha Mganga ameongeza kuwa wamezungumzia umuhimu
wa kuwahimiza watanzania kufuata sheria, na kwamba ofisi yake itatekeleza
wajibu wake bila kumuonea mtu.
Kiongozi Mwingine aliyekutana na Rais Magufuli ni
Mufti Mkuu wa Tanzania Sheikh Abubakar Zuber Ally ambaye pamoja na kumpongeza
Mheshimiwa Rais kwa juhudi kubwa alizoanza nazo katika uongozi wake, amesema
waislamu wote nchini wanamuunga mkono na kumuombea kwa Mwenyezi Mungu ili
aendelee na juhudi hizo.
"Na pia kwa niaba ya Waislamu tunataka
kumueleza kwamba kazi anayoifanya ni kazi ambayo tunairidhia na tunamuomba
aendelee kuifanya wala asiogope, na kauli yake ya Hapa Kazi Tu iendelee, kwa
sababu inaonesha kwamba sasa nchi yetu itakaa mahali pazuri" Alibainisha
Mufti Mkuu
Kiongozi Mwingine aliyekutana na Rais Magufuli ni
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Alhaji Abdallah
Majura Bulembo ambaye amempongeza Mheshimiwa Rais kwa kasi nzuri aliyoanza nayo
katika kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya Mwaka 2015- 2020 na kutaka kasi
hiyo iendelee.
Amesema Jumuiya ya Wazazi inaunga mkono kazi kubwa inayofanywa na Rais Magufuli na kwamba Mheshimiwa Rais amemuhakikishia kuwa ataendelea kufanya kazi hizo zaidi katika kutekeleza Ilani ya CCM.
Amesema Jumuiya ya Wazazi inaunga mkono kazi kubwa inayofanywa na Rais Magufuli na kwamba Mheshimiwa Rais amemuhakikishia kuwa ataendelea kufanya kazi hizo zaidi katika kutekeleza Ilani ya CCM.
"Tunafurahi kwamba yapo mambo mengi ambayo
Rais Magufuli ameanza kuyatekeleza kwa haraka, mojawapo likiwa ni kufutwa kwa
ada za shule, na hivi sasa wanafunzi watakwenda shule pasipo kutozwa ada"
alisisitiza Alhaji Bulembo
Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dar es salaam
04 Januari, 2016
0 comments:
Post a Comment