January 03, 2016

Kazi za usafi wa mazingira  kwenye maeneo tofauti Nchini zimefanyika ikiwa ni kuanza rasmi maadhimisho ya sherehe za kutimia miaka 52 ya Mapinduzi ya Zanzibar
Wananchi kadha wameonekana kuitikia vyema sughuli hiyo pamoja na vikosi vya ulinzi Nchini walishiriki.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alijumuika na Wananchi hao kwa kazi za usafishaji wa Mtaro wa maji machafu unaokusanya maji kutokea mitaa ya Muembe Njugu, Kwahani, Kariakoo, Kilimani na Kumalizikia Pwani ya Kilimani.
Wapiganaji wa Vikosi vya Mafunzo, Jeshi la Kujenga Uchumi, Kikosi Maalum cha Kuzuia Magendo, Zimamoto na Uokozi, Valantia, vikundi vya usafi wa mazingira vilivyomo  ndani ya Wilaya ya Mjini, watendaji wa Baraza la Manispaa na Wananchi walionekana kuhamasika katika harakati hizo.
Afisa Uhusiano wa Baraza la Manispaa  Zanzibar Moh’d Nassor Ali alieleza Baraza hilo limeanzisha mradi maalum wa kuimarisha Miundombinu katika uchimbaji wa mitaro { ZUSP } ndani ya Manispaa ya Mji wa Zanzibar wa lengo la kuujengea mazingira mazuri katika miendendo ya maji machafu.
Amesema hatua hiyo kwa hivi sasa inaendelea katika eneo la Mtaa wa Mpendae { Maarufu kwa Binti Hamrani } kwa ujenzi wa Mtaro mkubwa kazi inayokwenda sambamba na ujenzi wa mtaro kama huo katika Uwanja wa Michezo wa Mnazi Mmoja Mjini Zanzibar.
Akizungumza na washiriki wa zoezi hilo la usafi wa mazingira Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amewapongeza Wananchi pamoja na Vikosi vya ulinzi kwa ushiriki wao wa usafi wa mazingira.
Balozi Seif amesema  kwa vile Zanzibar imefanikiwa vyema katika kuangamiza Maradhi ya Malaria kwa asilimia 99% hakuna sababu  nguvu na hamasa kama hiyo  Wananchi kuchukuwa  juhudi ya kuielekeza katika usafi wa mazingira kwenye maeneo wanayoishi.
Katika kazi hiyo ya usafi wa mazingira kuanza rasmi kwa maadhimisho ya sherehe za kutimia Miaka 52 ya Mapinduzi ya Zanzibar ya Mwaka 1964 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alikabidhi zawadi ya vifaa tofauti vya usafi wa mazingira  kwa Kikundi cha usafi wa Mazingira cha Kilimani  { Kilimani City }.



0 comments:

Post a Comment