STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS
SECRETARY
PRESS
RELEASE
Zanzibar
03 Januari, 2016
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali
Mohamed Shein ametoa wito kwa wananchi wa Unguja na Pemba kujitokeza kwa wingi
kusherehekea maadhimisho ya miaka 52 ya Mapinduzi yanayoanza leo.
Dk. Shein amesema wananchi wana kila sababu za kushiriki
maadhimisho hayo kwa kuwa Mapinduzi ya tarehe 12 Januari, 1964 ndiyo yaliyoleta
Uhuru kwa wananchi wa Unguja na Pemba kutoka kwa wakoloni.
Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kushiriki zoezi
la kufanya usafi katika soko la matunda la Mombasa mjini Unguja leo, Dk. Shein
alisema wananchi wanaelewa vyema historia ya Mapinduzi ya Zanzibar na kwamba
wanajua wajibu wao katika kuyalinda na kuyadumisha.
Dk Shein alisisitiza kuwa “Kila mtu ana haki na wajibu wa
kuyaenzi na kuyaendeleza Mapinduzi ya mwaka 1964” kwa kuwa ni dhahiri hakuna
mwananchi asiethamini uhuru wake.
Rais wa Zanzibar aliwaeleza waandishi wa habari na wananchi
waliohudhuria zoezi hilo kuwa Mapinduzi ya mwaka 1964 yameleta maendeleo kwa
kila mwananchi na kwamba hakuna mwananchi asiyefaidika na matunda ya Mapinduzi.
Dk. Shein alisema Mapinduzi ya mwaka 1964 yalifanyika kwa
malengo maalum ya kuwakomboa wananchi Zanzibar kwa kuwa mazingira yaliyokuwepo
wakati huo kitendo cha kufanya Mapinduzi kilikuwa hakiwezi kuepukika.
Alibainisha kuwa wapo wanaoyakumbuka kwa furaha na wengine
wamenuna lakini Mapinduzi yalikuwa ni lazima na ndivyo ilivyofanyika na sasa
Zanzibar iko huru.
Aliwataka wananchi kushiriki katika ratiba mbalimbali za
maadhimisho hayo yakiwemo mashindano ya mpira wa miguu ya Kombe la Mapinduzi
yanayoanza leo katika uwanja wa Amaan Zanzibar.
Postal Address: 2422 Tel.+255 776 613 015, Fax: 024
2231822
0 comments:
Post a Comment