TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amemhakikishia
Waziri Mkuu wa Israel kuwa Serikali ya awamu ya tano ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania ipo tayari kushirikiana na kuimarisha zaidi mahusiano kati ya Tanzania
na Israel katika nyanja mbalimbali ili kuleta manufaa kwa pande zote.
Rais
Magufuli amesema hayo alipokutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Israel
hapa nchini mwenye makazi yake Mjini Nairobi - Kenya Mheshimiwa Yahel Vilan,
Ikulu Jijini Dar es salaam.
"Natambua mahusiano mazuri
yaliyopo kati ya Tanzania na Israel, mahusiano haya ni muhimu sana kwa ustawi
wa nchi zetu mbili, nataka mahusiano haya yaimarishwe zaidi "
Alisema Dkt. Magufuli.
Aidha,
Rais Magufuli ameahidi kuwa Tanzania itahakikisha inaanzisha ubalozi wake
nchini Israel haraka iwezekanavyo.
Kwa
upande wake Balozi wa Israel hapa nchini Mheshimiwa Yahel Vilan pamoja na
kumpongeza Rais Magufuli kwa kazi kubwa na nzuri iliyofanywa na uongozi wake
katika kipindi kifupi cha miezi miwili tangu aingie madarakani amemhakikishia
kuwa Israel itaendelea kushirikiana na Tanzania na ipo tayari kuimarisha zaidi
mahusiano.
Balozi
Vilan ametaja baadhi ya maeneo ya ushirikiano katika kiuchumi kuwa ni pamoja na
Kilimo, Maji, Ufugaji wa Nyuki na Sayansi na Teknolojia huku akibainisha kuwa
Israel imewaalika Jumuiya ya wafanyabiashara wa Tanzania kushiriki katika
Kongamano la biashara kati ya Tanzania na Israel litakalofanyika Mjini Tel Aviv
nchini Israel, mwezi Septemba mwaka huu.
Balozi
Vilan pia ameahidi kufikisha ujumbe wa Rais Magufuli kwa Waziri Mkuu wa Israel
Mheshimiwa Benjamin Netanyahu na pia ameahidi kuanzisha ofisi ya kutoa huduma ya
visa hapa nchini haraka iwezekanavyo.
Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU.
Dar es salaam.
19 Januari, 2016
0 comments:
Post a Comment