Waziri mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa amekutana na kufanya mazungumzo
na Balozi wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo anaemaliza muda wake, Bw.
Juma-Alfani Mpango.
Akizungumza na balozi Mpango ofisini kwake, Magogoni jijini Dar es
Salaam, Waziri Mkuu alimshukuru balozi huyo kwa pongezi zake na kumuomba
aendelee kuwa balozi mzuri wa kuitangaza Tanzania hata baada ya kurejea
nyumbani.
Pia alitumia fursa hiyo kuwaombea heri wananchi wa DRC pamoja na Rais
Joseph Kabila katika maandalizi ya uchaguzi mkuu ambao unatarajiwa kufanyika
nchini humo mwakani.
Kwa upande wake, Balozi Mpango ambaye alisema amekaa hapa nchini kwa
miaka 12, alimweleza Waziri Mkuu kwamba amejifunza mengi sana kutoka kwa
viongozi wa Tanzania kubwa vikiwa ni uchapakazi na unyenyekevu. “Nimeona
utawala wa Rais Benjamin Mkapa, Rais Jakaya Kikwete na sasa Dkt. John Pombe
Magufuli. Ninavutiwa na hatua mnazochukua hivi sasa katika kupambana na rushwa
na ufisadi,” alisema.
“Mambo niliyojifunza tangu nimekaa hapa ni uchapakazi na unyenyekevu.
Unaona kabisa kwamba mtu anaamini kuwa madaraka siyo kitu cha kujivunia kwa
mtumishi wa umma. Anachotakiwa kuwa nacho ni utayari wa kuwatumikia wananchi,”
alisema kwa Kiswahili sanifu.
Balozi Mpango aliomba mahusiano ya nchi hizi mbili yaendelezwe kwani
DRC imekuwa ikinufaika na matumizi ya bandari ya Dar es Salaam katika
kusafirishia bidhaa zake kwenda nchi za nje.
“Bandari ya Dar es Salaam ni muhimu sana kwetu. Mwaka 2004
tulisafirisha tani za mizigo 200,000, mwaka 2014 ziliongezeka na kufikia tani
milioni 1.3; na mwakani tunataraji zitaongezeka na kufikia tani milioni tatu,”
alisema.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Balozi
wa Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Kongo nchini,
Mhe. Juma - Alfani Mpango aliekwenda
ofisini
kwa Waziri Mkuu jijini Dar es salaam Desemba 2, 2015.
|
IMETOLEWA
NA:
OFISI YA
WAZIRI MKUU,
2 MTAA WA
MAGOGONI,
S. L.
P. 3021,
11410 DAR
ES SALAAM
JUMATANO,
DESEMBA 2, 2015.
0 comments:
Post a Comment