Wanawake 47 Zanzibar, wamepewa talaka na waume zao kutokana
na kushiriki kwao kupiga kura katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 25, mwaka
huu.
Wanawake hao walipewa talaka baada ya kutotii amri za
waume zao ambao waliwataka kutokwenda kupiga kura kutokana na kutofautiana kwa
itikadi za vyama.
Akizungumza na waandishi wa habari visiwani hapa mwishoni mwa
wiki, Mratibu wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (Tamwa), Ofisi
ya Zanzibar, Mzuri Issa, alisema katika uchaguzi huo ambao ulifutwa na
Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (Zec), wanawake wengi walikumbwa na
udhalilishaji wa kulazimishwa kupigia kura chama fulani kinyume na ridhaa yao.
Alisema Unguja na Pemba wanawake 47 walikatazwa kupiga
kura na walipoamua kwenda, waume zao waliwapa talaka na ndoa zao kuvunjika.
Aisha Mzuri alisema wanawake wengine 24 walitishiwa kupewa
talaka ikiwa watahudhuria mikutano ya kampeni ama watapiga kura na matokeo yake
hawakwenda kupiga kura.
“Wanawake wanne waliambiwa wasipige kura na walipiga kura,
lakini hawakuachwa, mmoja kati ya hao katelekezwa baada ya kukataa amri ya
kuhudhuria mkutano wa kampeni,” alisema Mzuri.
Aidha, alisema baadhi ya kauli za viongozi pia ziliwadhalilisha
baadhi ya wanawake ikiwamo kiongozi mmoja wa juu wa chama fulani alipokuwa
akihutubia mkutano wa hadhara wa kufunga kampeni za uchaguzi huko Gombani Pemba
alitoa kauli ya kumdhalilisha mwanamke.
Hata hivyo, alisema Tamwa kwa kushirikiana na wadau mbalimbali
ikiwamo kitengo cha wanawake katika Shirika la Umoja wa Mataifa (UN Women),
imetoa mafunzo kwa wanawake na wanaume 355 kutoka vyama 20 vya siasa. Alisema
wanawake 30 wamegombea nafasi za uwakilishi majimboni na 87 udiwani.
“Ni muhimu kufahamu kuwa kati ya hao wanawake 10 nafasi za
uwakilishi sawa na asilimia 33.3 na 20 wa udiwani sawa na asilimia 22.9,
wamefaidika moja kwa moja na mafunzo yaliyotolewa,” alisema.
Na Rahams Suleiman
0 comments:
Post a Comment