December 05, 2015

Serikali ya Ujerumani imeeleza kufurahishwa na kasi ya kupambana na rushwa na ufisadi ya Rais John Magufuli na kuahidi kumpa ushirikiano katika masuala ya maendeleo.
Ujerumani inakuwa nchi ya kwanza kuvutiwa na kasi ya Rais Magufuli  anae onekana kuelekeza nguvu katika   kupambana na maovu hayo na kuchochea maendeleo ya watu wenye kipato cha chini.
Aidha Ujerumani imesema inasubiri kuona vipaumbele vya maendeleo vitakavyoainishwa na serikali ya Rais Magufuli ili iweze kuisaidia utekelezaji.
Pongezi hizo zilitolewa jijini Dar es Salaam jana na Mkurugenzi wa Afrika, Wizara ya Mambo ya Nje ya Ujerumani, Georg Schmidt.
 Akizungumza na waandishi wa habari kuhusu ziara yake ya siku tano hapa nchini, Schmidt amesema katika kipindi cha mwezi mmoja tu Dk. Magufuli ameweza kushughulikia masuala muhimu ya kijamii ikiwamo kuboresha huduma za afya na kuwashughulikia wakwepa kodi.
Kasi ya Rais Magufuli, amesema, itasaidia kuokoa fedha nyingi ambazo zitakapokusanywa zitachangia miradi mbalimbali ya maendeleo kama alivyofanya tayari kwenye afya na elimu.
Mkurugenzi huyo amesema ziara yake nchini ilikuwa na lengo la kuangalia hali ya maendeleo nchini baada ya uchaguzi, miradi ya maendeleo inayotekelezwa na serikali yake pamoja na kukuza ushirikiano baina ya nchi mbili hizo.
Amesema ameshakutana na baadhi ya watendaji wa serikali, wabunge, wanaharakati, watendaji wa Jumuiya ya Afrika Mashariki pamoja na kuitembelea Mahakama ya Haki za Binadamu iliyopo mjini Arusha.
Akizungumzia suala la Zanzibar, Schmidt amewataka wananchi kuwa na subira wakati mazungumzo yakiendelea katika jitihada za kutatua mgogoro huo.
Amesema kwa sasa serikali ya Ujerumani itazielekeza fedha nyingi kwa serikali ya Tanzania ili kushughulikia wakimbizi kutoka Burundi wanaokimbia machafuko.

0 comments:

Post a Comment