Wahitimu wa Chuo cha Taaluma za Sayansi za Afya Zanzibar
wamehimizwa kuwa tayari kufanya kazi popote watakapopangiwa kwani wanawajibu
wa kuchangia jitihada Serikali katika kupambana na maradhi mbali mbali
yanayoisumbua jamii.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dr. Ali
Mohammed Shein ametoa rai hiyo katika Mahafali ya 22 ya Chuo cha Taaluma za
Sayansi za Afya Zanzibar huko Mbweni nje kidogo ya Mji wa Zanzibar katika hotuba
yake ilisomwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idi.
Amesema kuna baadhi ya baadhi ya wahitimu wanaoajiriwa na Wizara
ya Afya wanapiga chenga kufanya kazi Kisiwani Pemba wakisahau kwamba Wananchi
wa kisiwa hicho pia wanahitaji kupata huduma zao.
Amesema watumishi wa Umma wakiwemo wa sekta ya afya wanapaswa
kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia sheria na taratibu za kazi na miongozo
ya sehemu wanazoajiriwa na ni vizuri wawe mfano wa tabia njema kwa kushikamana
katika kutekeleza maadili ya kazi zao.
“ Nimefurahi kusikia kuwa katika orodha ya wahitimu wetu wa fani
za afya chuoni hapa wapo waliotoka Tumbatu, Kojani, Fundo, Mtende, na Maeneo
mengine ambayo watu wengi huwa wanaona tabu kwenda kufanya kazi kutokana na
mazingira ya Kijiografia yaliyopo “. Amesema Dr. Shein.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi pia aliiagiza
Wizara ya Afya kufanya tathmini ya mahitaji ya wataalamu wa afya katika maeneo
hayo ili kujua changamoto zilizopo na kuchukuwa hatua za haraka zitakazowezesha vijana kutoka maeneo hayo
kuajiriwa.
Akizungumzia suala la uwekezaji katika sekta ya Afya Zanzibar Rais
Shein amesema Serikali imekuwa ikishajiisha wawekezaji wa ndani na nje ya nchi
kuja kuwekeza katika sekta hiyo muhimu ili kusaidia katika kuimarisha huduma za
afya Nchini.
Rais wa Zanzibar amewasisitiza wahitimu wa Chuo cha Taaluma za
Sayansi za Afya Zanzibar kuchangamkia ajira zinazotolewa na Serikali na Sekta
Binafsi wakitambua kwamba Hospitali zote zina lengo la kuimarisha huduma za
afya kwa faida ya Wananchi.
Mapema Mkuu wa Chuo cha Taalum za Sayansi za Afya Zanzibar Dr.
Haji Mwita Haji amesema Uongozi wa Chuo hicho kupitia Baraza lake umeamua
kuongeza majengo zaidi ili kuwahudumia vyema wanafunzi wanaoamua kujiunga na
chuo hicho sambamba na mahitaji ya ongezeko la Hospitali na vituo vya Afya
Nchini.
Akimkaribisha Mgeni rasmi katika ufungaji wa Mahafali hayo ya 22
ya Chuo cha Taaluma za Sayansi za Afya Zanzibar, Naibu Waziri wa Afya Zanzibar
Mh. Mahmoud Thabit Kombo amewaomba wauguzi kufuata maadili ya kazi
zao ili kuondosha malalamiko yanayotolewa na wananchi juu ya lugha zao kwa
wagonjwa .
Jumla ya wahitimu 440 wamefanikiwa
kupata stashahada katika fani saba za sekta ya afya ikiwemo Afisa Tabibu wa
Afya ya Kinywa na Meno, Afisa Tabibu, Afya ya Mazingira, Uuguzi na Ukunga,
Utabibu wa Maabara,Madawa pamoja na Ufundi Sanifu wa Vifaa vya Hospitali.
0 comments:
Post a Comment