Serikali imezipongeza taasisi za elimu ya juu za umma na za
binafsi kwa kutoa fursa zaidi za masomo kwa vijana wa Zanzibar na kutoka nje na
kwamba hiyo ni hatua nzuri na muhimu kwa mustakabala wa Zanzibar.
Akizungumza katika mahafali ya 13 ya Chuo Kikuu cha Zanzibar
huko Tunguu nje kidogo ya mji wa Zanzibar, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa
Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesema ushirikiano wa sekta ya umma
na binafsi katika kuendeleza elimu nchini umeleta mafanikio makubwa.
“Serikali imefurahishwa kuona taasisi binafsi za elimu kuanzia
ngazi ya elimu ya awali hadi elimu ya juu zimeongezeka kwa kasi katika kipindi
cha miaka kumi iliyopita” alisema Dk. Shein na kuongeza kuwa taasisi hizo
zimekuwa msaada mkubwa kwa serikali.
Aliieleza jumuiya ya wanachuo na wageni waliohudhuria mahafali
hayo kuwa ameridhishwa kuona kuwa kumekuwepo na ongezeko kubwa la vijana wa
Zanzibar wanaojiunga na elimu ya juu ndani na nje ya nchi na kueleza kuwa huo
ni mwelekeo mzuri kwa taifa.
“Naupongeza sana mwamko huu wa vijana kuchangamkia elimu ya juu
kwa kuwa ni ukweli ulio wazi kuwa elimu ni msingi wa taifa bora na lenye ustawi
hivyo naamini kwa dhati kuwa mustakabala wa Zanzibar unategemea hizi jitihada
zetu katika kuwaelimisha vijana” Dk. Shein alisisitiza.
Katika mnasaba huo ameushukuru uongozi wa Chuo Kikuu cha
Zanzibar kwa kuongeza udhamini wa nafasi za masomo kwa vijana wa Zanzibar
kutoka 55 hadi 100 kwa mwaka na kueleza kuwa huo ni mfano unaopaswa kuigwa na
taasisi nyingine za elimu ya juu nchini.
Dk. Shein alibainisha kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
inathamini mchango wa taasisi za elimu ya juu nchini katika maendeleo ya
Zanzibar na watu wake kwa taasisi hizo kuendelea kutoa wahitimu bora ambao
wameweza kupata mafanikio katika sehemu mbalimbali wanazotekeleza wajibu wao.
Katika hotuba yeka hiyo, Dk. Shein alisisitiza kuwa pamoja na
kuwepo mafanikio katika kujenga mazingira bora na ya usawa kati ya watoto wa
kike na wa kiume katika elimu, Serikali itaendelea kuchukua hatua zas
kuimarisha mazingira hayo ili kutoa fursa zaidi kwa watoto wa kike.
“Serikali imeweka mikakati ya kuimarisha hali ya wanawake
kielimu, afya na kuwa uwezo kwa madhumuni ya kulinda haki na kutoa fursa kwa
wanawake kote nchini katika harakati za maendeleo ya kiuchumi na kijamii” Dk.
Shein alisisitiza.
Alibanisha kuwa baadhi ya matunda ya hatua hizo ni namna ambavyo
vijana wa kike wanavyopata fursa za kujiunga kwa wingi na elimu kuanzia ngazi
ya chini hadi elimu ya juu na wamekuwa wakionesha uwezo mkubwa ambapo mara kwa
mara wamekuwa wakishika nafasi za juu kuliko vijana wa kiume.
Kwa upande wa wahitimu amewataka kuitumia vyema elimu waliyopata
kwa kutumia fursa zilizopo za kujipatia kipato na zaidi wajiandae kukabiliana
na changamoto za maisha.
“Muzichukue changamoto kama fursa kwenu kwani zitawasaidia
kuwajenga na kuongeza uwezo kwa kuwa maisha ni safari iliyojaa changamoto
ambazo kila mwanadamu anapaswa kujiandaa kukabiliana nazo” Dk. Shein aliwasihi
wahitimu hao.
Katika mahafali hayo jumla ya wahitimu wahitimu 678 wa ngazi ya
vyeti (254), Diploma (33), 349 shahada za kwanza na 42 shahada za uzamili
katika fani mbalimbali walitunukiwa vyeti vyao na Mkuu wa Chuo hicho ambaye pia
ni Mwenyekti wa Bodi y Wadhamini ya Chuo Profesa Suleiman Bin-Nasry Basahal.
Akizungumza katika mahafali hayo Makamu Mkuu wa Chuo hicho
Profesa Mustafa Roshash, alieleza kuwa uongozi wa chuo unaendelea na jitihada
zake za kuimarisha taaluma chuoni hapo kwa kuendelea kusomesha wakufunzi wake katika
kiwango cha shahada za uzamivu.
Alibainisha kuwa chuo hicho kinatoa kozi 8 ngazi ya cheti, 8
ngazi ya diploma, 14 ngazi ya shahada ya kwanza, shahada za uzamili 4 na moja
ya Uzamivu.
Profesa Roshash alieleza pia kuwa wanafunzi chuoni hapo wanatoka
Zanzibar,Tanzania Bara na nchi za Malawi, Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi,
Zambia, Botswana, Ethiopia, Sudan, Nigeria na Afrika Kusini.
Alifafanua kuwa tangu kuanzishwa kwake chuo hicho mwaka 1998,
kimetoa wahitimu 5791 kati yao wahitimu 3042 ni wanaume ambao ni asilimia 52
wakati wahitimu waliobaki 2749 ambao ni asilimia 48 ni wanawake.
0 comments:
Post a Comment