![]() |
Mkurugenzi Mkuu wa kampuni hodhi ya rasilimali za reli Tanzania (RAHCO) Mhandisi Benhadard Tito (kulia) |
TAARIFA
KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa Jamhuri ya
Jamhuri wa Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amemsimamisha kazi
Mkurugenzi Mkuu wa kampuni hodhi ya rasilimali za reli Tanzania (RAHCO)
Mhandisi Benhadard Tito ili kupisha uchunguzi wa kina kufuatia ukiukwaji mkubwa
wa taratibu za manunuzi uliobainika katika mchakato wa utoaji wa zabuni ya
ujenzi wa reli ya kati.
Akitoa taarifa kwa vyombo
vya habari, Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue amesema, Rais Magufuli
amefikia uamuzi huo baada ya kuitisha kikao cha wataalamu kutoka Wizara na
Taasisi mbalimbali za serikali ambazo zinahusika katika utekelezaji wa Mradi wa
Ujenzi wa Reli ya kati kwa kiwango cha kisasa yaani "Standard Gauge"
Amesema pamoja na
kumsimamisha kazi Mkurugenzi Mkuu wa RAHCO, Rais Magufuli ameivunja bodi ya
RAHCO baada ya kujiridhisha kuwa haikutekeleza ipasavyo wajibu wake katika
kusimamia mchakato wa zabuni hiyo na badala yake imeonekana kutetea
kilichofanyika
Aidha Rais Magufuli
amemtaka Mkurugenzi Mkuu wa RAHCO Mhandisi Benhadard Tito kutoa ushirikiano kwa
vyombo vya serikali vitakavyofanya uchunguzi zaidi kuhusu mchakato wa Zabuni
hiyo.
Pia ameiagiza Mamlaka ya
udhibiti wa manunuzi ya umma (PPRA) kuchunguza na kuchukua hatua dhidi ya
kampuni za ukandarasi zilizopewa zabuni ya ujenzi huo endapo itathibitika kuwa
zimeshiriki katika ukiukwaji wa sheria.
Katika hatua nyingine
Balozi Sefue amesema, Rais Magufuli amevunja bodi ya Mamlaka ya Reli Tanzania
(TRL) kutokana na kutoridhishwa na jinsi bodi hiyo ilivyoshughulikia ripoti ya
uchunguzi wa mchakato wa ununuzi wa mabehewa ya treni.
Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
0 comments:
Post a Comment