JAMHURI YA MUUNGANO WA
TANZANIA
KURUGENZI YA MAWASILIANO YA RAIS, IKULU
SALAAM
ZA MHE. JOHN POMBE MAGUFULI, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, KWA
WANANCHI KATIKA KUMBUKUMBU YA MIAKA 54 YA UHURU, TAREHE 09 DESEMBA, 2015.
Namshukuru Mwenyezi
Mungu aliyeiwezesha nchi yetu kutimiza miaka 54 ya uhuru kwa salama na amani.
Namshukuru Mungu pia kwa kuniwezesha kuiona siku hii nikiwa Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania. Napenda kuchukua fursa hii, kuwapongeza Watanzania
wenzangu kwa Taifa letu kutimiza 54 ya Uhuru tarehe 09 Desemba, 2015. Napenda
kuwahakikishia kwamba, kama ilivyokuwa kwa Serikali za awamu zilizopita,
Serikali ya Awamu ya Tano itafanya kila lililo ndani ya uwezo wake kuhakikisha
kwamba Uhuru, Amani na Umoja na wa Taifa letu hauchezewi na mtu, kikundi au Taifa
lolote. Tutaendelea kudumisha Uhuru wetu
na Mapinduzi ya Zanzibar, tunu ambazo ni msingi wa Muungano wetu na Utanzania
wetu.
Tofauti na
ilivyozoeleka tumeamua mwaka huu kusherekea kumbukumbu hizi kwa kufanya kazi,. Wakati
tunapata Uhuru Taifa letu lilikuwa likiongozwa na kauli mbiu ya UHURU NA KAZI.
Kauli hii ilikuwa na lengo la kuamusha moyo na uzalendo wa kufanya kazi
miongoni mwa Watanzania kwa kutambua kuwa uhuru wetu hautakuwa na maana kama
hatutafanya kazi kwa juhudi na maarifa ili kujenga Taifa linalojitegemea. Watanzania
katika miaka ile waliitikia wito huo kwa kufanya kazi za kuwaongezea kipato na
za kujitolea katika kuunga mkono juhudi za Serikali za kuwaletea maendeleo.
Katika miaka ya hivi karibuni moyo na uzalendo wa kufanya kazi miongoni mwetu
umepungua sana. Kwa sababu hiyo, niliamua kutumia siku ya kumbukumbu za uhuru
wetu mwaka huu kukumbushana na kutekeleza kwa vitendo kauli mbiu ya UHURU NA
KAZI kwa kufanya kazi hususan ya usafi wa mazingira. Madhimisho ya Uhuru
mwakani yatasherehekewa kama kawaida.
Nawapongeza viongozi
wa Mikoa na Wilaya na wa Taasisi za umma na binafsi na mashirika yasiyo ya
kiserikali yaliyojitokeza katika kuhakikisha kuwa zoezi la usafi wa mazingira
linafanikiwa.
Napenda kutoa
wito kwa Halmashauri zote nchini kuhakikisha zinaweka mifumo na taratibu
thabiti zitakazowezesha usafi wa miji yetu kuwa endelevu. Viongozi wa Mikoa, Wilaya
na Halmashauri waache visingizio, uwezo na mamlaka ya kuhakikisha kwamba usafi
katika miji yao unadumishwa wanao. Uwezo wa utendaji wao utapimwa pia kutokana
na hali ya usafi wa miji yao.
Naomba wananchi tushirikiane
katika kuhakikisha kuwa nyumba na mazingira ya nyumba zetu yanakuwa safi na
maji ya kunywa katika maeneo ambayo hayawekwi dawa yanachemshwa. Aidha, wananchi
wajizuie kutupa taka ovyo na viongozi wa Serikali za mitaa, vijiji na vitongoji
wahakikishe kwamba kila nyumba inakuwa na choo. Tutashinda vita dhidi ya
maradhi kama kipindupindu ikiwa sote tutazingatia kanuni za afya. Kila mtu
atimize wajibu wake.
Mwalimu alisema
Uhuru na Kazi na mimi nasema Hapa Kazi Tu.
0 comments:
Post a Comment