Mahakama ya Wilaya ya Ilala, Dar es Salaam,
imemhukumu askari polisi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, G 9762 PC Daniel
(24) kutumikia kifungo cha maisha jela, baada ya kupatikana na makosa ya kubaka
na kumlawiti mtoto wa miaka 13.
Mbali na kifungo hicho, mtuhumiwa huyo
ameamriwa kulipa fidia ya Sh milioni 2 ili iwe fundisho kwa watu wengine wenye
tabia kama hizo.
Hukumu hiyo ilitolewa jana na Hakimu Mkazi
Mwandamizi Mfawidhi, Said Mkasiwa baada ya kukamilika ushahidi uliowasilishwa
mahakamani hapo na upande wa mashtaka uliokuwa na mashahidi wanne.
“Mahakama inatoa hukumu kwa mtuhumiwa
kutumikia kifungo cha miaka 30 kwa kosa la kubaka na kutumikia kifungo cha
maisha jela kwa kosa la kulawiti mtoto na baadaye atalipa fidia ya Sh 2,000,000
ili iwe fundisho kwa wengine wenye tabia kama hizo,” alisema Mkasiwa.
Katika utetezi wake, mtuhumiwa kupitia
kwa wakili wake ambaye alitajwa kwa jina moja la Manzi, alidai kosa hilo ni la
kwanza na ni kijana mdogo ambaye ni nguvu kazi ya taifa, pia
alifanya kosa hilo akiwa amelewa, hivyo hakujua alichokuwa akikifanya.
Awali Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Elik
Shija, alidai hakukuwa na kumbukumbu za makosa ya nyuma dhidi ya
mshtakiwa, hivyo aliiomba mahakama hiyo kutoa adhabu kali kwa mtuhumiwa ili iwe
fundisho kwa wengine wenye tabia kama hiyo.
0 comments:
Post a Comment