December 30, 2015

WAJUMBE wa kamati tendaji ya hifadhi ya mkondo wa Pemba ‘PECA’ wametakiwa kuharakisha kuibua maeneo yenye samaki wa matumbawe, ili kuyahifadhi kupitia mradi wa usimamizi wa uvuvi Kusini Magharibi ya bahari ya hindi ‘SWIOfish’ unaofadhaliwa na benki ya dunia.
Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa Idara ya maendeleo ya uvuvi Zanzibar, Mussa Aboud Jumbe alipokua akizungumza na wajumbe hao kwenye mkutano uliofanyika Kiwanda cha makonyo Wawi Chakechake Pemba wakati wa kuwasilisha mradi huo.
Alisema kazi kubwa kwa hatua za awali wa wajumbe hao wa kamati tendaji, ni kukaa na wavuvi katika vijiji vyao, ili kujua wana aina gani ya samaki na kisha mradi huo kuanza utekelezaji wa kuwahifadhi.
Jumbe alieleza kuwa ujio wa mradi wa ‘SWIOfish’ ni kuendeleza yale yalioachwa na mradi wa MACEMP, ingawa kwa mradi huo mpya wa zaidi ya miaka 15, unalenga zaidi katika uhifadhi wa samaki moja kwa moja.
Alisema PECA kwa Pemba, Menei na Mnemba kwa Unguja ndio maeneo ambayo mradi huo umelenga utekelezaji wake, ambapo kazi ya wajumbe wa kamati tendaji wa taasisi hizo ni kubainisha maeneo yanayohitajia kuhifadhiwa.
Kwa upande wake Mratibu wa mradi huo Zanzibar, Ramla Talib Omar alisema kwa awamu ya kwanza mradi unatelezwa nchi tatu Mozambique, Comoro na Tanzania ambapo baadae nchi nyengine zitajumuisha.
Katibu wa PECA Pemba Khamis Sharif, alisema kama mradi huo utatekelezwa kama maandiko yalivyo, unaweza kuleta matunda makubwa kwenye sekta ya uvivi Zanzibar.
Nae mwenyekiti wa wavuvi wilaya ya Micheweni Mkubwa Said Ali alisema suala la kuyahifadhi maeneo yenye samaki hasa wa matumbawe ni jambo jema.
Mradi huo wa ‘SWIOfish’ unaofadhiliwa na benki ya dunia, tayari uliazna tokea Juni mwaka huu, ambapo kwa hatua za awali Tanzania ikiwemo Zanzibar utatekelezwa miaka sita na kisha kuendelea kwa awamu ya pili.






Haji Nassor, Pemba

0 comments:

Post a Comment