December 02, 2015

Mkurugenzi Mwendeshaji wa Shirika la Biashara la Taifa Zanzibar ZSTC Mwanahija Almas Ali amesema Maendeleo ya Sekta ya Zao la Karafuu inaendelea kuimarika zaidi Zanzibar hasa baada ya kuanzishwa kwa Mfuko wa Maendeleo ya Karafuu.
Akizungumza na Waandishi wa Habari Makao Makuu ya ZSTC Maisara Bi. Mwanahija alisema Mfuko huo ulianzishwa kuongeza nguvu jitihada za Serikali za kuimarisha zao hilo la uchumi wa Taifa.
Alisema utafiti ulifanyika juu ya namna ya kufanya mageuzi yenye tija katika Sekta ya Karafuu ndipo ikaoneka umuhimu wa kuanzisha Mfuko huo ambapo muda mfupi baada ya kuanzishwa unaonekana kuleta faida katika uimarishaji wa zao hilo.
“Madhumuni ya kuanzishwa kwa Mfuko wa Maendeleo ya Karafuu ni kuhakikisha Sekta ya Karafuu inakua na kuimarika zaidi. Kuongeza idadi ya mikarafuu na uzalishaji ambapo hivi sasa Wananchi wamehamasika zaidi katika upandaji mikarafuu kwa wingi”. Alifahamisha Bi. Mwanahija.
Alisema Mfuko huo ambao upo chini ya Mkurugenzi Mwendeshaji wa Shirika la ZSTC umejipanga kufanya sensa ya mikarafuu sambamba na kuwasajili Wakulima na Wafanyabiashara wa zao hilo ili kurahisisha upatikanaji wa huduma.
Aidha alifahamisha kuwa kupitia Mfuko huo na kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo na Maliasili kutafanyika tafiti kwenye kila eneo linayohusu zao la karafuu kwa lengo la kugundua changamoto na kuzifanyia kazi.
Alisema Shirika la ZSTC kwa kushirikiana na Wadau wengine inakamilisha mpango maalumu wa kuziongezea hadhi na thamani karafuu za Zanzibar kupitia mradi wa ‘Branding’ ili kuongezeka kwa uzalishaji kwenda sambamba na kuongezeka kwa tija kwa Wakulima na Taifa.
Alisema hivi sasa mpango huo upo katika kutafuta vinasaba vinavyoonyesha ubora wa karafuu za Zanzibar kupitia Mkemia Mkuu wa Serikali Zanzibar.
Alisema kupitia Mfuko huo Shirika limeongeza jitihada za kutoa elimu kwa Wakulima juu ya uchumaji na uanikaji unaotakiwa ili kulinda ubora wa zao hilo katika soko la nje.
Alisema Mfuko huo umekuwa ni msaada mkubwa katika uimarishaji wa zao la karafuu hasa kwa Wakulima ambapo unatoa fidia kwa Wakulima wanaopata ajali wakati wa uchumaji kupitia Shirika la Bima Zanzibar.
Alifahamisha kuwa Mfuko huo umelipa bima ya milioni 60 kwa Shirika la Bima ili kuwafidia Wakulima 100 wanaokisiwa kupata ajali katika zoezi la uchumaji wa karafuu mwaka 2015/2016 ambapo hadi sasa tayari watu tisa wameripotiwa kupata ajali wote kutoka Pemba.
Alisema Wakulima wanaendelea kupata mikopo ya uchumaji kupitia Mfuko huo na alifahamisha kuwa katika bajeti ya 2015/2016 Mfuko umepanga kutumia milio 140 kwa ujenzi wa barabara ya Ng’omeni ikiwa ni msaada wa kusadia miundombinu ya sehemu za uzalishaji wa karafuu.
Akizungumzia makadirio ya mavuno ya karafuu ya mwaka 2015/2016 Mkurugenzi huyo alisema Shirika limekadiria kununua tani 2800 mpaka 3200 katika mwaka huo.



:Pili Khatib na Zuhura Omar, MUM

0 comments:

Post a Comment