Karafuu ni zao linalotokana na mkarafuu, ingawa karafuu
hazimo katika kundi la vyakula wala vinywaji lakini ni kiungo na dawa muhimu
sana kwa maisha ya binadamu.
Mikarafuu ilianza kupandwa kwenye visiwa vya Shelisheli,
Mauritius na sehemu nyinginezo katika karne ya 19. Miche ya mikarafuu ililetwa
Zanzibar kutoka Indonesia, mashariki ya mbali mwaka 1818.
Mikarafuu inastawi zaidi Visiwani vya Unguja na Pemba ambapo
katika miaka 30 iliyopiata Zanzibar ilikuwa inazalisha asilimia 80 ya karafuu
zote zinazohitajika duniani ambapo uchumi wake ulitegemea sana zao la karafuu.
Karafuu zina matumizi mengi, ambapo hutumika kama kiungo
katika vyakula na vinywaji, dawa kwa maradhi ya tumbo, meno na misuli vile vile
hutumika katika kuleta harufu nzuri ya kinywa, mwili na mazingira ya nyumbani.
Pia karafuu zinatumika katika uzalishaji wa bizaa nyengine
ikiwemo sigara, mafuta ya karafuu ambayo hutumika kwa kuchulia misuli inayouma,
kutengezea dawa za meno na perfume kwa ajili ya manukato.
Karafuu zinatumika sana kwenye mapishi ya vyakula
mbali mbali ikiwemo nyama, biriani, pilau, mchuzi wa masalo na vyakula vikavu
kama vile vileja, beskuti na donas na kwa ubande wa vinywaji karafuu hutumika
katika chai na maziwa .
Kama vilivyo viungo vyengine karafuu nazo zina utamu, ladha
na harufu nzuri ya kuvutia na kupendeza katika vyakula hivyo ambapo watu wengi
hasa katika bara la Asia, Mashariki ya kati na ulaya hupenda sana kiugo cha
karafuu katika vyakula vyao.
Karafuu inasaidia usagaji mzuri wa chakula tumboni na ni
nzuri kwa matibabu ya maumivu ya tumbo, tumbo kujaa gesi na
kiungulia. Hivyo karafuu ni miongoni mwa kiungo muhimu katika vyakula kutokana
na vinasaba vya aina ya eugnol vilivyomo ndani ya karafuu.
Aidha karafuu hutumika katika utengenezaji wa mafuta (Mafuta
ya karafuu) ambapo mafuta hayo husafisha damu, tafiti zinaonyesha kuwa visanaba
vilivyomo katika karafauu vinapunguza sumu katika damu. Vinasaba aina ya eugnol
vilivyomo ndani ya karafuu vinasaidia mzunguko mzuri wa damu.
Kutokana na ukuaji wa viwanda duniani kumekuwa na mahitaji
makubwa ya karafuu pamoja na kuongezeka kwa nchi zinazozalisha ambapo karafuu
hutumika sana kwa utengenezeji wa sigara katika nchi za Ulaya, Asia na
Marekani.
Sigara zinazotengenezewa karafuu kutoka Zanzibar zina
thamani na ubora zaidi duniani kuliko sigara zinazotengezewa karafuu kutoka
nchi nyengine kutokana na ubora wa karafuu za Zanzibar.
Pia karafuu hutumika katika viwanda kwa ajili ya kutengezea
dawa za meno kwa ajili ya kutunza meno na kuondosha maumivu ya meno na ufidhi,
kung’arisha meno na kuleta harufu nzuri ya kinywa, harufu iliyomo katika
karafuu inasaidia kuondosha harufu mbaya mdomoni.
Kwa mujibu wa utafiti uliochapishwa mwaka 2011katika Jarida
la Asia Plant Science and Research toleo namba 1 (2) karafuu husadia kutibu
vidonda vya mdomo na kuimarisha Afya ya fizi pamoja na kuzuia meno kuoza.
Aidha Mafuta ya karafuu yamekusanya vinasaba vya eugnol
ambavyo vimekuwa vikitumiwa na Madaktari wa meno kwa miaka mingi kutibu
matatizo ya meno na ufizi.
Karafuu inatumika katika urembo ambapo hutumika kusugulia
mwili (scrub) kwakuchanganya unga wa karafuu kavu iliyosagwa na mafuta ya nazi
na liwa ambapo husuguliwaa mwili mzima kuondoa uchafu.
Mbali na hayo pia karafuu hutengenezewa sabuni ambazo ni
nzuri kwa kuondosha maradhi ya ngozi kama vile harara, vipele na chunusi na
kuifanya ngozi iwe nyororo na yenye kuvutia. Sio hayo tu lakini pia karafuu
hutumika kutengenezea mafuta mazuri kwa sababu karafuu ina harufuu ya kipekee
inayovutia.
Hivyo karafuu na mafuta ya karafuu ni mazuri kwa ajili ya
kutunza ngozi hasa kwa ngozi yenye mabaranga, mba na kuchakaa ambapo huifanya
ngozi kuwa nzuri na yenye kung’ara.
Matumizi ya karafuu na mafuta ya karafuu kwa kawaida
humfanya mtu kuwa mchangamfu kwa kuondoa uchofu kwa vile karafuu inaiweka akili
katika hali nzuri na kufanya ubongo ufanye kazi vizuri. Pia husadia kuondoa
matatizo ya kusinzia, kupoteza kumbukumbu na wasiwasi.
Mafuta ya karafuu husaidia kuondosha maumivu ya kichwa kwa
kuchanganganywa na chumvi na kupakaa kwenye paji la uso hupoza maumivu. Pia
huondosha matatizo katika mfumo wa upumuaji na kusafisha koo na hutibu
kikohozi, mafua na pumu.
Mchanganyiko wa mafuta ya karafuu na mafuta ya ufuta (sesame
oil) ni mazuri kwa kuondsha maumivu ya sikio.
:Zuhura Omar na Pili Khatib -MUM
0 comments:
Post a Comment