TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Tokea yalipofanyika Mapinduzi ya tarehe 12
Januari, 1964, tumekuwa tukiadhimisha tukio hilo kubwa katika historia ya
Zanzibar kila mwaka inapofika siku hiyo. Tukio hilo kubwa ndilo lililopelekea
kutangazwa kwa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar na Rais wa kwanza wa Zanzibar,
Marehemu Mzee Abeid Amani Karume.
Chama
Cha Wananchi (CUF) kimekuwa kikishiriki kikamilifu katika maadhimisho ya siku
hiyo kila mwaka kwa kutambua kwamba Mapinduzi ya tarehe 12 Januari, 1964 ni
Mapinduzi ya Wazanzibari wote. Malengo makuu ya Mapinduzi hayo yameelezwa na
kufafanuliwa vyema kupitia Dikrii Nam. 6 ya mwaka 1964 iliyopitishwa na Baraza
la Mapinduzi ambayo yanatajwa kwamba ni kuleta usawa, umoja na maridhiano baina
ya Wazanzibari wote na kupiga vita aina zote za ubaguzi.
Tayari
tumetangaziwa kwamba kuanzia tarehe 2 Januari, 2016 kutakuwa na shughuli mbali
mbali zenye lengo la kuadhimisha Mapinduzi yetu na hatimaye, kama ilivyo ada na
desturi, kufikia kilele tarehe 12 Januari, 2016 katika sherehe ambazo
zitafanyika Uwanja wa Amaan, mjini Zanzibar.
CUF kama chama cha siasa kinawatakia kheri
Wazanzibari wote katika kuadhimisha miaka 52 ya Mapinduzi yao.
Hata hivyo, tunatambua kwamba sherehe za mara hii
zinafanyika wakati ambapo nchi yetu na watu wake wema wamo katika mtihani
mkubwa kufuatia kitendo cha mtu mmoja, Jecha Salim Jecha, kuamua kwa utashi
wake na waliomtuma kuiingiza nchi yetu katika msukosuko na taharuki kwa kudai
kwamba eti ameufuta uchaguzi mkuu wa tarehe 25 Oktoba, 2015 na matokeo yake.
Kwa kitendo hicho cha mtu mmoja ambaye amevunja Katiba, amevunja Sheria ya
Uchaguzi na amevunja hata maadili ya kazi yake, mara hii nchi yetu itaadhimisha
Mapinduzi huku Serikali ikiwa inaongozwa na viongozi ambao hawana uhalali na
ridhaa ya wananchi.
CUF tumesisitiza mara zote kwamba hatukubaliani
na uamuzi huo wa mtu mmoja kujinyakulia mamlaka ya wananchi wa Zanzibar
yaliyowekwa kikatiba. Kwa msingi huo huo, tunapenda kutumia fursa hii kuwaeleza
wananchi wa Zanzibar kwamba viongozi wetu hawatoshiriki katika shughuli
walizopangiwa katika ratiba ya sherehe hizi kwa sababu zifuatazo:
Kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984
(Toleo la 2010), Ibara ya 28, Ibara ya 42(2), Ibara ya 48(b), Ibara ya 90(1) na
Ibara ya 92(1) Serikali iliyokuwepo madarakani na Baraza la Wawakilishi
lililokuwepo katika kipindi cha miaka mitano iliyopita (2010 – 2015) vilimaliza
muda wake wa uongozi tarehe 2 Novemba, 2015 kwa upande wa Serikali na tarehe 12
Novemba, 2015 kwa upande wa Baraza la Wawakilishi. Kwa sasa, hatuna viongozi
wenye uhalali wa kikatiba kuweza kutekeleza majukumu ya kiserikali. Kwa hivyo,
kushiriki katika ratiba hizo kwa kutumia nafasi ambazo hazina uhalali tena wa
kikatiba ni kwenda kinyume na dhamira ya waasisi wa Mapinduzi, jambo ambalo
hatuko tayari kulifanya.
Kiuataratibu,
kilele cha sherehe huongozwa na Rais ambaye yupo kikatiba. Kwa mara ya kwanza
tokea tarehe 12 Januari 1964, sherehe za miaka 52 zitaongozwa na Rais ambaye
ameshamaliza muda wake wa uongozi kikatiba na ambaye hana uhalali na ridhaa ya
wananchi wa Zanzibar. Kushiriki katika sherehe hizo ni kuhalalisha kipindi cha
uongozi ambacho hakipo tena kikatiba. Maalim Seif Sharif Hamad na viongozi
wenziwe ndani ya Chama waliokuweko Serikalini hadi tarehe 2 Novemba, 2015
hawako tayari kuhalalisha uvunjaji wa Katiba ya Zanzibar ambayo ndiyo sheria
kuu ya nchi.
Viongozi
wa CUF wakiongozwa na Maalim Seif Sharif Hamad wanaamini katika msingi mkuu wa
Mapinduzi ya tarehe 12 Januari, 1964 chini ya uongozi wa Baba wa Taifa la
Zanzibar, Marehemu Sheikh Abeid Amani Karume, ambao ni kuleta utawala wenye
ridhaa ya wananchi walio wengi. Msingi huo umewekwa wazi na kutiliwa nguvu na
Katiba ya Zanzibar ya 1984 (Toleo la 2010) kupitia Ibara ya 9(2)(a) ambapo inaelezwa
kwamba, “Mamlaka ya kuendesha nchi ni ya wananchi wenyewe ambapo nguvu na uwezo
wote wa Serikali kufuatana na Katiba utatoka kwa wananchi wenyewe.”
Mamlaka
hayo ya wananchi yalitekelezwa tarehe 25 Oktoba, 2015 kwa kuwachagua viongozi
watakaoongoza Serikali yao kwa miaka mitano ijayo. Kitendo chochote cha
kupindua mamlaka hayo ya wananchi ni kwenda kinyume na misingi ya Mapinduzi na
misingi iliyowekwa na Baba wa Taifa la Zanzibar, Marehemu Sheikh Abeid Amani
Karume. CUF hatuko tayari kushiriki katika kuisaliti misingi hiyo na kuisaliti
dhamira ya Mzee Karume.
4.
Sherehe za kuadhimisha Mapinduzi ya tarehe 12 Januari, 1964 zina lengo la
kukumbuka malengo ya Mapinduzi hayo na dhamira ya waasisi wake wakiongozwa na
Marehemu Sheikh Abeid Amani Karume katika kusimamia utawala wenye ridhaa ya
wananchi walio wengi. Kuzitumia sherehe za Mapinduzi kuhalalisha utawala usio
na ridhaa ya wananchi wa Zanzibar na ambao haupo kikatiba ni usaliti mkubwa wa
dhamira ya kuwepo kumbukumbu hiyo. CUF hatuko tayari kuwa sehemu ya usaliti
huo.
Kwa
sababu hizo zilizoelezwa hapo juu, viongozi wa CUF hawatoshiriki katika ratiba
walizopangiwa mpaka pale chaguo la wananchi wa Zanzibar walilolifanya tarehe 25
Oktoba, 2015 litakapoheshimiwa.
Tuweke
wazi kwamba tulichoamua ni viongozi wetu kutoshiriki katika ratiba
zinazohusisha viongozi wa Serikali ambao wamemaliza muda wao wa uongozi. Kwa
hivyo, bado tunachukua nafasi hii kuwatakia wananchi wa Zanzibar maadhimisho
mema ya miaka 52 ya Mapinduzi na kuwataka waendeleze umoja, mshikamano na amani
katika nchi.
Mwisho kabisa, tunamuomba Mwenyezi Mungu awalaze
mahala pema Peponi muasisi wa Mapinduzi yetu, Marehemu Mzee Abeid Amani Karume,
na waasisi wenzake wote na awasamehe makosa yao.
Tunawaomba Wazanzibari wote kila mmoja kwa dini
yake wamuombe Mwenyezi Mungu kuijaalia kheri na salama nchi yetu na
kuyasimamisha yaliyo ya haki. Tukiishika kamba ya Mwenyezi Mungu hatutoanguka.
Tunawatakia wote kheri ya mwaka mpya wa 2016 na
tunaamini unakuja na kheri kubwa kwa Zanzibar na watu wake. Ni mwaka ambao
safari ya ujenzi wa Zanzibar Mpya itaanza.
MAPINDUZI DAIMA
HAKI
SAWA KWA WOTE
MANSOOR YUSSUF HIMID
MSHAURI WA KATIBU MKUU – CUF
MSHAURI WA KATIBU MKUU – CUF
31 DESEMBA, 2015
0 comments:
Post a Comment