TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amekutana naMakamu
wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Mgombea Urais wa
Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharrif Hamad, leo tarehe 21 Desemba, 2015 Ikulu
Jijini Dar es Salaam kufuatia maombi
yake ya siku nyingi.
Mazungumzo
ya Viongozi hao pia yamehudhuriwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan.
Viongozi
hawa kwa pamoja wamejadili hali ya kisiasa Zanzibar na wamefurahishwa na hali
ya usalama na utulivu inayoendelea. Aidha, Mhe. Rais Magufuli amewapongeza Rais
wa Zanzibar Mhe. Dkt. Ali Mohamed Shein, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, na
viongozi wote wanaoshiriki katika mazungumzo ya kuleta hali ya uelewano
Zanzibar.
Rais
Magufuli pia amewapongeza na kuwashukuru
wananchi wa Zanzibar kwa kudumisha amani na utulivu wakati wa mazungumzo baina
ya viongozi wa CUF na CCM yakiendelea huko Zanzibar.
Katika
Mazungumzo hayo Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar Maalim Seif Sharrif Hamad amemueleza Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania juu ya hali ya siasa Zanzibar kadiri anavyoielewa yeye na Rais
Magufuli amemshukuru Makamu huyo wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar kwa taarifa yake
nzuri huku akimsihi waendelee na mazungumzo hadi suluhisho muafaka lipatikane.
Majadiliano
yanayoendelea yanatoa fursa ya kudumishwa kwa utulivu na sifa njema ya nchi
yetu. Wote kwa pamoja wamewaomba wananchi waendelee kuwa watulivu ili kutoa
nafasi ya majadiliano yanayoendelea kufikia hatma njema. Wameelezea matumaini
yao kuwa vyama vya CCM na CUF haviwezi kushindwa kupata suluhu ya mgogoro huo.
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amemuhakikishia kuwa Serikali ya Jamhuri ya
Muungano itahakikisha kuwa amani na utulivu unaendelea kudumishwa Zanzibar.
Gerson
Msigwa
Kaimu
Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU.
21Desemba, 2015
0 comments:
Post a Comment