TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI.
Itakumbukwa kuwa Desemba 27, mwaka 2015,
Kamati Maalum ya Halmashauri Kuu ya CCM ya Taifa Zanzibar ilikutana, chini ya
Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi ambaye pia ni Rais wa Zanzibar na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Ali Mohamed Shein.
Kama ilivyo ada, mara tu baada ya
kumalizika kwa mkutano huo, Chama Cha Mapinduzi Zanzibar kupitia Msemaji wake
Mkuu kilipata nafasi ya kuzungumza na Waandishi wa Habari, kwa madhumuni ya
kuwajuvya kwa muhtasari maamuzi yaliyofikiwa na kikao hicho.
Aidha, Chama Cha Mapinduzi
kimesikitishwa sana na taarifa iliyotolewa na Kaimu Mkurugenzi wa Habari na
Mawasiliano ya Umma wa Chama cha CUF Ismail Jussa kwa kukariri na kuripoti
mazungumzo ya ndani ya kikao chetu, chenye dhamana ya kuendesha na kusimamia
masuala yote ya siasa kwa upande wa Zanzibar.
CCM kinamshangaa kiongozi huyo kwa
kuacha kuyazungumzia mambo yanayohusu chama chake na badala yake kuanza
kufuatilia mambo ya ndani ya CCM ni dhahiri kwamba kiongozi huyo anavyoonyesha
jinsi gani alivyoishiwa na kufilisika kisiasa.
Chama Cha Mapinduzi kinachukua nafasi
hii kuwaomba Viongozi na Wanachama wote wa CCM na wapenda Amani na Utulivu wa
nchini kuzipuuza na kuzidharau porojo (drip) hizo za kisiasa za wapinzani
zilizokosa heshima, hekima, busara, maadili na uvumilivu wa kisiasa na badala
yake waendelee na shughuli zao za kujiletea maendeleo zitakaowapatia mapato
halali na kujikwamua na umasikini.
Aidha, waelekeze nguvu zaidi katika
kudumisha suala zima la amani na utulivu huku wakisubiri maelekezo kutoka
Vyombo vya Kisheria hususan Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar kutangaza siku ya
uchaguzi wa marudio, na kujiweka tayari na hatimaye kujitokeza kwa wingi siku
hiyo tayari kwa kuwaipigia kura wagombea wote wa CCM.
Kama hiyo haitoshi, Chama Cha Mapinduzi
kinasikitishwa na kinalaani vikali taarifa hiyo iliyotolewa na Jussa ambayo kwa
hakika inaendeleza makosa ya kutoa matokea ya uchaguzi ya Chama chake (CUF)
ilhali akijua kuwa Uchauguzi huo tayari ulishafutwa na Tume halali na
iliyowekwa kikatiba na hivyo kuwafanya Wazanzibari wajiulize masuala yasiyopata
majibu sahihi kwamba Jussa haoni kufanya hivyo sio tu ni kwenda kinyume na
sheria za nchi bali pia ni kosa la jinai.
Mwisho kabisa, Chama Cha Mapinduzi kamwe
haitaingilia maamuzi ya chama chochote cha kisiasa kwani chama hichi (CCM) ni
kikubwa, kilichojijengea heshima kubwa kwa wananchi wa Tanzania, Barani Afrika
na Duniani na kubwa zaidi ni chama pekee kinaheshimu demokrasia.
Ahsanteni.
………………
(Waride Bakari Jabu),
Katibu wa Kamati Maalum ya NEC,
Idara ya Itikadi na Uenezi - CCM,
ZANZIBAR.
(Waride Bakari Jabu),
Katibu wa Kamati Maalum ya NEC,
Idara ya Itikadi na Uenezi - CCM,
ZANZIBAR.
0 comments:
Post a Comment