Watu wasiojulikana
wamezichoma moto Eka Mia 150 za miwa katika Mashamba ya zao hilo ya Kiwanda
cha Sukari Mahonda na kusababsisha hasara inayokadiriwa kufikia Shilingi za Kitanzania Bilioni
1.8.
Moto huo
ulioshambulia mashamba hayo jana majira ya saa sita mchana ulizimwa kwa
muda wa saa tatu kwa ushirikiano kati ya wapiganaji wa Kikosi cha Zima moto na
Uokozi Zanzibar, JKU, Wafanyakazi wa Kiwanda cha Sukari Mahonda pamoja na
Wananchi .
Makamu wa Pili wa Rais wa
Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amefika katika shamba hilo kuangalia hali halisi
ya hasara iliyopatikana ambapo Meneja wa Mradi wa Kiwanda hicho Tushar
Mehta amesema eneo hilo la Eka hizo lilikuwa na uwezo wa kuzalisha Sukari Tani
Mia 750 zenye thamani ya Shilingi Bilioni 1.5.
Tushar amesema
amesikitishwa na kitendo cha watu waliofanya hujuma ya kuchoma miwa hiyo iliyokuwa ishapea licha ya Kiwanda hicho kuwekeza mradi huo wenye lengo la kuongeza mapato
kwa Serikali na kuongeza fursa za ajira kwa wakaazi wa maeneo jirani
yanayokizunguuka.
Kwa upande wake Makamu wa
Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amesema kitendo cha kuchomwa
shamba hilo la miwa Mahonda unapaswa kualaaniwa kwa vile kimeleta sura mbaya na
kuisababishia ukosefu wa mapato Serikali.
Ameuomba Uongozi wa
Kiwanda cha Sukari Mahonda kutovunjika moyo na kuahidi Serikali kupitia
vyombo vyake vya Dola inaendelea na uchunguzi kumbaini Mtu au kikundi
kilichohusika na vitendo hicho na kufikishwa kwenye vyombo vya Sheria.
0 comments:
Post a Comment