Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimeipongeza Serikali
ya Awamu ya Tano chini ya uongozi wa Rais, Dkt.John Pombe Magufuli, Makamu wa
Rais, Samia Suluhu Hassan na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa Kassim kwa kasi nzuri
waliyoanza nayo katika utekelezaji wa Ilani ya Chama hicho.
Kutokana na Kikao cha Kamati Kuu ya Halmashauri
Kuu ya CCM Taifa kilichofanyika Desemba 07, 2015 jijini Dar es Salaam chini ya
Mwenyekiti wa CCM, Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Jakaya
Mrisho Kikwete, kikao hicho kilipokea taarifa juu ya utendaji wa Serikali
katika utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015-2020.
Akitoa pongezi hizo kwa niaba ya Chama, Katibu Mkuu wa CCM, Ndugu Abdulrahman
Kinana amesema Kamati Kuu imeunga mkono hatua zinazochukuliwa na Serikali ya
Awamu ya Tano katika kuhakikisha Ilani ya Uchaguzi ya Chama hicho kwa
mwaka 2015-2020 inatekelezwa kwa ufanisi.
Pia, Kinana amesema Kamati Kuu ya Chama inapongeza
na kuunga mkono juhudi kubwa zinazofanywa na Serikali katika kusimamia vyanzo
vya mapato ya Serikali ikiwa ni kuhakikisha Mamlaka ya Mapato(TRA) na Mamlaka
ya Bandari Nchini(TPA) zinasimamia ukusanyaji wa kodi za Serikali ipasavyo.
Hata hivyo, Kinana amesema pamoja na
kuunga mkono na kupongeza kasi waliyoanza nayo, Rais Magufuli, Makamu wa Rais
na Waziri Mkuu, Kamati Kuu inawataka viongozi wengine wote kuiga mfano
huu mzuri na kuhakikisha wanatimiza wajibu wao ipasavyo.
Na Bakari Issa Madjeshi.
0 comments:
Post a Comment