December 08, 2015


Wananchi wanaoishi karibu na eneo lililotengwa kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya Rufaa katika kijiji cha Binguni, Wilaya ya Kati Unguja  wameanza kulivamia eneo hilo  kwa shughuli za ujenzi wa nyumba za kuishi.
Eneo hilo la ekari 80 Wizara ya Afya linakusudiwa kujengwa Hospitali hiyo kubwa pamoja na  nyumba za wafanyakazi.
Mkuu wa Mkoa Kusini Unguja Dkt. Idrissa Islam Hija amesema wananchi wamekuwa watukutu kufuata sheria za nchi na kila wanalofanya ni haki yao licha ya hatua za  kuwaelimisha na kuwazuilia kuchukuliwa.
Amesema hayo katika ziara ya kuliangalia eneo hilo la wizara ya afya iliyofanywa na uongozi wa Wizara ya Afya ukiongozwa na Naibu Waziri wa Wizara hiyo  Mahmoud Thabit Kombo.
Mkuu wa Mkoa amesema eneo hilo limepimwa rasmi na Serikali kwa ajili ya matumzi ya Wizara hiyo hivyo matumizi mengine yeyote yatakayofanywa hayatatambuliwa na uongozi wa Mkoa.
Amewataka wananchi wanaoishi karibu kutolitumia kwa shughuli yeyote ya ujenzi ili kujiepusha na hasara inayoweza kuwapata baadae.
Dkt. Idrissa Islam Hija ameishauri Wizara ya Afya kuanza hatua ya kulizungushia uzio ili wananchi wasipate mwanya wa kulivamia.
Aidha amewataka masheha na madiwani wa eneo la Binguni kutotowa vibali vinavyowaruhusu wananchi kujenga kwani uzoefu unaonyesha  watu wanaovamizi  maeneo kwa kujenga nyumba hupatiwa vibali na masheha ama madiwani.
“Madiwani na Masheha hamuruhusiki kutoa vibali vya  matumizi ya ardhi na kufanya hivyo ni kosa jiepusheni na tabia hiyo hasa katika eneo hili lilitengwa kwa ajili ya shughuli za Serikali,” amesisitiza Mkuu wa Mkoa.
Naibu Waziri wa Afya Mahmoud Thabit Kombo ameuagiza uongozi wa Wilaya ya Kati na Mkoa wa Kusini Unguja kuwazuiya wananchi wawili walioanza ujenzi katika eneo hilo  na kuwataka  kuvunja  nyumba hizo haraka iwezekanavyo.
Amesema iwapo  watashindwa kuvunja  majengo hayo wenyewe Wizara itasimamia kuvunja nyumba hizo na  watalalipia gharama zote.



       


Maelezo Zanzibar  

0 comments:

Post a Comment