Mamlaka ya Mapato
Tanzania (TRA) imefanikiwa kukusanya kodi ya zaidi ya shilingi bilioni tano
kutoka kwa wafanyabiashara waliokuwa wamekwepa kulipa kodi.
Akiongea na waandishi
wa habari leo jijini Dar es Salaam Kaimu Kamishna Mkuu wa TRA Dkt. Philip
Mpango amesema hatua hiyo imekuja kufuatia agizo kutoka kwa Waziri Mkuu Mhe.
Kassim Majaliwa Kassim alipofanya ziara ya kushtukiza katika Bandari ya Dar es
Salaam Novemba 27 mwaka huu.
Katika Maagizo hayo
ya Mhe.Kassim aliitaka TRA kubaini wamiliki wa makontena 329 yaliyoondolewa
kwenye bandari kavu kinyume na taratibu pamoja na kutaja bidhaa zilikuwemo
ndani ya kontena hizo ikiwemo wakwepaji wa kodi na kuwachukulia hatua watumishi
wa TRA walihusika katika mchakao huo.
Aidha Dkt. Mpango
aliongeza kwa kusema mpaka sasa wamefanikiwa kubaini jumla ya kampuni 43
zilizohusika katika uigizaji wa makontena ambayo yaliondolewa katika bandari
kavu kinyume na taratibu.
“Katika kontena
tulizozikamata hizo tumekuta bidhaa za matairi ya magari,samani
mbalimbali,betri za magari,vifaa vya ujenzi,nguo na bidhaa mchanganyiko”
alisema Kamishna Mpango.
Kwa upande wa
watumishi wa TRA mpaka sasa watumishi 35 wa ngazi mbalimbali wamesimamishwa
kazi wakiwemo 27 waliokamatwa wiki hii katika geti namba 5 ambao wanashikiliwa
na Jeshi la Polisi kwa mahojiano na uchunguzi zaidi.
Pia aliendelea
kufafanua kuwa Uongozi wa TRA unawataka watumishi wote kuorodhesha mali zao ili
kuhakiki uhalali wa mali hizo na endapo watabainika kuwa wamezipata mali hizo
kinyume na sheria hatua stahiki zitachukuliwa dhidi yao.
Naye Naibu Kamishna
Mkuu Lusekelo Mwaseba ameeleza kuwa kwa sasa TRA inapitia kwa upya taratibu za
utoaji wa leseni ili kuondoa mianya pamoja na kuweka udhibiti katika uondoshaji
wa mizigo katika bandari zote,ICDs na bohari za forodha.
“Sambamba na
kufuatilia taratibu hizo,TRA pia itahakikisha inawafuatalia mawakala wote wa
forodha walioshiliki katika upotevu wa makontena na kuwachukulia hatua ikiwemo
kuwafungia leseni na adhabu nyingine kulingana na sheria zilizowekwa” alisema
Mwaseba.
Kaimu Kamishna Mkuu
Mpango alitoa wito kwa wote wanaohusika na uondoshwaji wa makontena kutoka
bandari kavu kinyume na taratibu kujitokeza na kulipa kiasi cha kodi yote
wanayodaiwa kama ilivyoagizwa na Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania
Mhe.Dkt.John Pombe Magufuli aliaagiza kwamba wadaiwa wote walipe madeni yao
ndani ya siku saba baada ya hapo watachukuliwa hatua kufuatana na mujibu wa
sheria.
0 comments:
Post a Comment