November 20, 2015

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli amehudhuria hafla fupi iliyoandaliwa kwa ajili ya wabunge katika viwanja vya Bunge Mjini Dodoma na kuagiza fedha zilizochangwa kwa ajili ya kugharamia hafla hiyo zipelekwe Katika Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa ajili ya kununulia vitanda vya wagonjwa. 
Mheshimiwa Magufuli ametoa agizo hilo baada ya kupokea taarifa kuwa wadau mbalimbali wamechanga kiasi cha shilingi milioni 225 kwa ajili ya kugharamia hafla ya wabunge katika siku ya uzinduzi wa Bunge. 
Dkt Magufuli amesema alipata taarifa za kuwepo kwa michango hiyo ya fedha na kutoa maelekezo hayo ili zikatumike kupunguza tatizo la wagongwa wanaolala chini kutokana na uhaba wa vitanda unaikabili hospitali hiyo.
“kwa kufanya hivyo tutakua tumejinyima sisi wenyewe lakini tutawanufaisha wenzetu wenye matatizo makubwa yanayoweza kutatuliwa kwa fedha hizo”. 
 Awali akitoa taarifa ya michango hiyo Ofisa wa Spika wa Bunge Said Yakubu amesema kati ya shilingi milioni 225 zilizochangwa ni shilingi milioni 24 tu ndio zilizotumika katika hafla hiyo baada ya kuzingatia maagiza ya Rais Magufuli. 
Rais Magufuli amekabidhi vyeti vya kutambua mchango wa wadau waliochangia fedha wakiwemo Benki za NMB, CRDB na Benki ya Afrika pamoja na Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ya PSPF na PPF. 

0 comments:

Post a Comment