Waandishi wa habari
Zanzibar wametakiwa kufuata maadili na miongozo ya taaluma zao bila ya kujali
vikwazo na changamoto zinazowakabili katika utendaji wa majukumu yao.
Hiyo ni hatua ya
kuifanya jamii iendelee kuunga mkono juhudi zinazofanywa na waandishi hao
katika nyanja mbali mbali za kiuchumi, kijamii na kisiasa.
Mkuu wa Chuo cha
Uandishi wa Habari Zanzibar, Dkt. Aboubakar Sheikh Rajab amesema kuwa endapo
waandishi wa habari watashindwa kuzingatia maadili yao kutokana na changamoto
za kiutendaji fani hiyo itapoteza thamani na heshima yake ya kujenga jamii na maendeleo
ya nchi.
Akizungumza katika
mkutano wa wadau wa Klabu ya waandishi wa habari Zanzibar ZPC ameeleza kuwa
kuna baadhi ya waandishi wa habari wanatumiwa vibaya na baadhi ya vyama vya
kisiasa katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu jambo ambalo ni kinyume na misingi ya
maadili yao.
" Waandishi lazima kwanza tufikie wakati
tutambue kuwa asili ya kazi yetu ni kujitolea kwa jamii licha ya kuwa hali zetu
za kipato ni ndogo lakini tusikubali wanasiasa na watu wenye uwezo kutumia
udhaifu huo kutusababisha tuvunje maadili yetu.
Akitoa mada ya umuhimu
wa waandishi wa habari kuzingatia maadili ya uandishi wa habari na utangazaji,
Katibu Mkuu wa Tume ya Utangazaji Zanzibar Chande Omar Omar amesema waandishi
wa habari wanaofuata maadili wanakuwa na fursa pana ya kuepuka vikwazo na
lawama kutoka kwa jamii.
" Mnatakiwa kujua
kuwa hamfanyi kazi kwa ajili yenu bali mnafanya kazi kwa ajili ya jamii nzima
hivyo ujumbe mnaotoa kupitia vyombo nyenu kwanza mkae na kuupitisha katika
tanuru la kitaaluma na maadili badae ndiyo mpate kuutuma kwa jamii.
“Mnatakiwa kuepuka
masuala ya udini,ukabila,utaifa,rangi ya mtu jinsia na hali ya kiuchumi na
kijinsia bali kila kundi mlipe haki yake kwa lengo la kuhakikisha Zanzibar
inaendelea kuwa nchi yenye amani na utulivu wa kupigiwa mfano.",alisema
Omar.
Kwa upande wake
mshiriki wa mkutano huo, mwakilishi kutoka Chama cha TADEA Zanzibar, Juma Ali
Khatib amewataka waandishi wa habari kutumia kalamu zao kufafanua kwa kina
upotoshwaji wa sheria unaofanyika Zanzibar kwa sasa tangu Tume ya uchaguzi
nchini ilipofuta matokeo ya uchaguzi mkuu.
Mkutano huo umefikia maazimio
ni pamoja na waandishi wa habari Zanzibar kuendelea kufuata maadili ya fani
hiyo kwa wakati wote na kuhamasishana kusoma Katiba za nchi pamoja na sheria
mbali mbali ili waweze kuwa na uelewa mpana wa masuala ya kisheria wanapotoa
taarifa zao.
Is-haka Omar,
Zanzibar.
0 comments:
Post a Comment