November 21, 2015


TAMKO LA TAASISI ZA KIISLAM ZANZIBARTAASISI ZA KIISLAM ZANZIBAR


Ndugu waandishi wa habari,
Assalam alaykum,

Awali ya yote tunawashukuru kwa kuitikia mualiko wetu ambapo pamoja na kupata taarifa hii mapema lakini kwa kuthamini wito wetu mumeacha shughuli zenu na mumefika. Ahsanteni. Lengo la mkutano wetu huu ni kutoa taarifa kuhusu ushiriki wa Taasisi za Kiislam Zanzibar zisizokuwa za Kiserikali katika Mchakato Mzima wa Uchaguzi Mkuu Zanzibar uliofanyika Jumapili tarehe 25-10-2015.
Ndugu waandishi wa habari, Taasisi za Kiislam Zanzibar kwa kuona kuwa zina wajibu pia wa kusimamia masuala yanayohusu maendeleo ya nchi yetu ziliamua kuangalia Mchakato Mzima wa Uchaguzi Mkuu Zanzibar katika hatua zote kupitia kikundi chao kinachotambulika Kikundi cha Waangalizi cha JUMAZA ambacho kilipewa kibali na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar. Kikundi chetu kiliangalia uchaguzi katika majimbo yote 54 ya uchaguzi Unguja na Pemba. Kwa kuwa kutangaza matokeo, kuyapokea na kuyakubali ni hatua muhimu katika uchaguzi wa kidemokrasia, kabla ya kukamilika kutangazwa matokeo yote ya urais wa Zanzibar.
Kikundi chetu tarehe 27-10-2015 kilitoa taarifa kwa vyombo vya habari iliyobeba mambo matatu muhimu; kwanza Tume kuwa waadilifu kwa kutangaza matokeo ya kweli yanayoaminika ambayo yanatokana na matakwa ya Wazanzibari, wagombea wa urais hasa wa vyama vikuu vya CUF na CCM kuwa waungwana kwa kuyakubali matokeo yatakayotangazwa na Tume. Aidha, tuliwaomba wananchi kuwa watulivu na kuendelea kuwa na subra wakati matokeo yanaendelea kutangazwa na Tume.
Ndugu waandishi wa habari, hata hivyo kama ilivyotokea kwa waangalizi wengine wa ndani na nje, kikundi chetu pia kilipatwa na mshangao mkubwa kwa hatua aliyoichukua Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi siku ya Jumatano tarehe 28-10-2015 kufuta uchaguzi wote wa Zanzibar baada ya kukamilisha kutangaza matokeo ya urais katika majimbo 31. Baada ya tukio hili kikundi chetu kilitoa taarifa yake ya awali mapema iwezekanavyo ambapo pamoja na kasoro ndogo ndogo zilizojitokeza kikundi chetu kiliona kuwa Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar uliofanyika tarehe 25-10-2015 ulikuwa wa uwazi, uhuru, amani, haki na uadilifu na kukidhi viwango vya kimataifa vya uchaguzi bora.
Ndugu waandishi wa habari, kama munavyojua hatua ya kufutwa uchaguzi imepelekea Mgogoro mwengine wa kisiasa na kikatiba Zanzibar na kuifanya nchi yetu kukosa muelekeo hadi leo baada ya uchaguzi na hivyo kuzusha wasi na khofu kwa wananchi wengi. Athari za hali hii zilijitokeza mapema kwa kupanda sana bei za vyakula muhimu na hivyo kuongeza mzigo na makali ya maisha kwa wanyonge wa Zanzibar. Katika mazingira haya, Taasisi za Kiislam za Zanzibar zimechukua hatua kadhaa katika kusaidia kufikia suluhu na kuikwamua nchi yetu hapa ilipo zikiwemo; kwanza tarehe 6-11-2015 Taasisi zetu ziliwaandikia barua za kukutana na viongozi wakuu wa nchi wakiwemo Mheshimiwa Ali Hassan Mwinyi, Mheshimiwa Dr. Amani Abeid Karume, Mheshimiwa Dr. Ali Mohamed Sheni, Mheshimiwa Seif Sharif Hamad na Mheshimiwa Balozi Seif Ali Iddi ili tuwaombe wakutane kwa majadiliano ya suluhu na maridhiano.
Hatahivyo, bahati mbaya pengine kutokana na kutingwa na mambo haikuwezekana kukutana na mheshimiwa hata mmoja. Baada ya kushindikana kuonana nao tuliamua kutumia njia mbadala ya kuwapelekea nasaha zetu kwa njia ya maandishi. Kwa ujumla nasaha zetu zililenga kuwaomba waheshimiwa kuwa na nia safi katika kutafuta suluhu ya kudumu, kuweka mbele maslahi makubwa ya nchi badala ya binafsi pamoja na kuwa waadilifu.
Aidha, katika hatua nyengine siku ya tarehe 9-11-2015 Taasisi zimewapelekea barua Mabalozi wa nchi sita waliopo Tanzania ambazo ni Marekani, Uingereza, Ujerumani, Ufaransa, Norway na Sweeden. Maudhui ya barua zetu kwa mabalozi ni kuwaomba kutusaidia katika kufikia suluhu hasa kwa kuwa nchi zao ndizo zinazosimamia utekelezaji wa Mfumo wa Kidemokrasia ikiwemo chaguzi huru, za wazi, amani na zinazoweka mbele matakwa ya wapiga kura.
Mwisho tunawaomba Wazanzibari wote kuwa na subra na kuendelea kutunza amani tuliyonayo, kuwa watulivu, kuendelea kuiombea dua nchi yetu pamoja na kusubiri matokeo ya mazungumzo yanayoendelea ya kutafuta suluhu na ufumbuzi.

Ahsanteni kwa kutusikiliza.

............................................
MUHIDDIN ZUBEIR MUHIDDIN

KATIBU MTENDAJI – JUMAZA 

0 comments:

Post a Comment