Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi CUF Maalim Seif Sharif Hamad,
amerejea kauli yake ya kutotambua kufutwa kwa uchaguzi mkuu wa Zanzibar
uliofanyika tarehe 25 mwezi uliopita.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam mara
baada ya kikao cha mashauriano na viongozi wa Umoja wa Katiba ya Wananchi
UKAWA, Maalim Seif amesema kinachohitajika na kuendelea na mchakato wa kuhakiki
kura zilizobakia na mshindi kutangazwa.
Kuhusu tamko lililotolewa na serikali juu ya kufutwa rasmi kwa
uchaguzi huo kupitia tangazo lililochapishwa kwenye gazeti rasmi la serikali mapema
wiki hii Maalim Seif amesema tamko hilo limekosa uhalali tangu lilipotolewa na
Mwenyekiti wa ZEC Bw
Jecha Salim Jecha .
Maalim Seif ambaye pia ni Mgombea Urais wa
Zanzibar kupitia CUF amesema Chama chake hakijalizingatia tamko hilo na wala
hakijadili uwezekano wa kurejewa kwa uchaguzi huo, kwa madai kuwa uchaguzi
ulikamilika bila ya kuwepo malalamiko kutoka chama chochote cha siasa na wala
Tume ya Uchaguzi.
Mapema akizungumza baada ya kikao hicho cha mashauriano,
aliyekuwa mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chadema Mhe.
Edward Lowassa amesema kikao hicho kilichojadili Mkwamo wa kisiasa Zanzibar
kimekwenda vizuri.
Hata hivyo amesema ufafanuzi zaidi utatolewa Jumapili ijayo
ambapo viongozi hao wanakusudia kuzungumza na waandishi wa habari jijini Dar es
Salaam.
Kabla ya kikao hicho Maalim Seif alifanya mazungumzo na Balozi
wa Umoja wa Ulaya (EU) Bw. Filberto Seregondi katika hoteli ya Serena jijini
Dar es Salaam na kuelezea hatua zinazochukuliwa kukwamua mkwamo wa kisiasa
Zanzibar.
Balozi Seregondi ambaye anamaliza muda wake wa utumishi hapa
nchini, aliambatana na ujumbe wa waangalizi wa uchaguzi mkuu wa Tanzania kutoka
Umoja huo.
Hassan Hamad, OMKR
0 comments:
Post a Comment