November 14, 2015

Spika  wa Bunge la 11 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, anatarajiwa kuchaguliwa mjini Dodoma Jumanne ijayo, ratiba ya Bunge hilo imeeleza.

“Kutokana na kuitishwa kwa Bunge na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk John Pombe Joseph Magufuli.
Ofisi ya Bunge inapenda kuwatangazia wabunge wote wateule kuwa wanatakiwa kuwasili mjini Dodoma Novemba 13, 2015 (jana) tayari kwa ajili ya usajili” imeeleza ratiba hiyo iliyowekwa katika ukurasa wa Facebook wa Bunge.

Kwa mujibu wa ratiba hiyo, kuanzia jana mpaka kesho, wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, watapaswa kuwa wameshawasili mjini Dodoma na kujisajili kwa watumishi wa Bunge.

Ratiba ya Bunge hilo imeonesha kuwa siku ya Jumatatu, ya kesho kutwa wabunge wote wanatarajiwa kuwa wamekamilisha usajili ili kushiriki kikao cha maelekezo katika Ukumbi wa Bunge kitakachohusisha kutembelea ukumbi huo kuanzaia saa nne asubuhi

Ratiba hiyo inaonesha kuwa siku hiyo hiyo kuanzia saa 10 jioni, wabunge hao watakuwa na mikutano ya vyama vyao, ambako inatarajiwa hoja kubwa itakuwa jina la Spika na Naibu Spika.

Siku ya Jumanne wiki ijayo, Kikao cha Kwanza cha Bunge la 11 mkoani Dodoma kitaanza kitakachotanguliwa kwa kusomwa kwa tamko la Rais Magufuli la kuitisha Bunge.

Mara baada ya kusomwa kwa tamko hilo kutafuatiwa na uchaguzi wa Spika, mara baada ya kiongozi huyo  kupatikana anatarajiwa kuanza kuapisha wabunge na kazi hiyo ataendelea nayo hadi siku ya Alhamisi asubuhi.

Siku ya Alhamisi ya Novemba 19 Rais Magufuli anatarajiwa kupeleka kwa Spika jina la Waziri Mkuu saa 10 jioni ili kuthibitishwa na wabunge wote kwa kura.

Baada ya kuthibitishwa kwa Waziri Mkuu, pia siku hiyo hiyo atachaguliwa Naibu Spika na baadae  siku ya Ijumaa Rais Magufuli atatoa hotuba yake ya kwanza kwa bunge na kuahirishwa kwa Bunge.

0 comments:

Post a Comment