May 17, 2014


STATE HOUSE ZANZIBAR

OFFICE OF THE PRESS SECRETARY

PRESS RELEASE

    Zanzibar                                                               17 Mei , 2014

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesema uhusiano mzuri wa kisiasa na kidiplomasia uliopo kati ya Zanzibar na Vietman unatoa fursa ya kipekee ya kuuimarisha kwa kupanua maeneo mapya ya ushirikiano kwa kuhusisha sekta binafsi.
 Amesema Zanzibar inayo mengi ya kujifunza kutoka Vietnam hasa katika sekta za kilimo, uvuvi na utoaji huduma sekta ambazo zimeifanya nchi hiyo kuwa miongoni mwa nchi zilizopata mafanikio makubwa ulimwenguni.

Akizungumza na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kisoshalisti ya Vietnam Nguyen Phuong Nga Ofisi Kwake Ikulu leo, Dk. Shein alieleza kuwa amefurahishwa na hatua iliyofikiwa ya mazungumzo ya ushirikiano katika sekta ya kilimo na uvuvi ambayo ni sehemu ya matokeo ya ziara yake nchini Vietnam Novemba mwaka 2012.

Alibainisha kuwa matokeo ya timu ya Serikali ya Vietnam iliyofika nchini kufuatia ziara yake hiyo yataweka misingi madhubuti wa ushirikiano katika nyanja hizo na hatimae kusaidia kufikia lengo la Serikali la kujitosheleza kwa chakula hususan mchele kama lilivyo katika Mkakati wa kujitosheleza chakula nchini.
“Nimefurahi kusikia kuwa mazungumzo yamefikia hatua nzuri kuhusu ushirikiano kati ya nchi zetu katika nyanja za kilimo na uvuvi na ninaamini kuwa mazungumzo hayo yatatoa matokeo mazuri kwa manufaa ya Serikali na wananchi wa nchi zetu” Dk. Shein alimueleza Naibu Waziri huyo na kuongeza kuwa Zanzibar ina ari kubwa ya kujifunza kutoka Vietnam ili kufikia azma yake ya kufanya mapinduzi ya kijani.

Sambamba na ushirkiano katika ngazi za Serikali Dk. Shein alisisitiza kuwa fursa ya uhusiano huo mzuri ambao umeanza mapema miaka ya sitini haina budi kutumika kwa kutoa nafasi kwa sekta binafsi za nchi mbili hizo kushiriki katika biashara na uwekezaji ili kuimarisha zaidi udugu na urafiki kati ya Serikali na wananchi wa Zanzibar na Vietnam.

 Mbali na sekta za uvuvi na kilimo Mhe Rais alihimiza ushirikiano kati ya nchi hizo katika sekta ya utalii na huduma ambazo zote nchini Vietnam zimeonesha kuimarika na kusisitiza kuwa milango iko wazi kwa wawekezaji na wafanya biashara wa Vietnam kufanya shughulizi zao Zanzibar.
Dk. Shein alimueleza Naibu Waziri huyo kuwa ziara yake nchini Tanzania imedhihirisha urafiki na udugu wa kweli kati ya Tanzania na Vietnam na kuongeza kuwa Tanzania ingependa kuona ukaribu wa wananchi wa nchi mbili hizo unaimarika zaidi.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Vietnam Nguyen Phuong Nga alieleza kuwa Serikali na wananchi wa nchi yake  wanajivunia na kuthamini uhusiano na urafiki wake na Serikali na wananchi wa Tanzania na kwamba imekuwa bahati kwake kupata fursa kufanya ziara humu nchini.
Kwa hiyo alisema kuwa kuna kila sababu ya kuimarisha uhusiano huo na kukubaliana na rai aliyoitoa Mheshimiwa Rais ya kutumia mazingira mazuri ya uhusiano wa kisiasa na kidiplomasia uliopo kati ua nchi hizo kupanua maeneo ya ushirikiano.

Alibainisha kuwa ziara yake nchini Tanzania imelenga katika kuhakikisha kuwa uhusiano kati ya Vietnam na Tanzania unaimarika.

0 comments:

Post a Comment