April 15, 2014


STATE HOUSE ZANZIBAR

OFFICE OF THE PRESS SECRETARY

PRESS RELEASE

Zanzibar

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesisitiza umuhimu wa Wizara na Idara za Serikali kuzingatia vipaumbele katika matumizi ya fedha za umma hususan yanapokuja masuala yanayowagusa wananchi.

Dk Shein amesema hayo leo wakati wa Mkutano wa kujadili Taarifa ya Utekelezaji wa Mpangokazi wa Wizara ya Afya katika kipindi cha Robo ya Tatu ya Mwaka wa Fedha 2013/2014.

“Tunahitaji kuwa makini zaidi wakati tunapopanga matumizi ya fedha katika wizara na kwa wakurugenzi hawana budi kuhakikisha kuwa maeneo yao ya kipaumbele hasa yale yanayogusa wananchi moja kwa moja yanapewa umuhimu wa kwanza” Dk. Shein alieleza.

Katika mkutano huo Dk. Shein alieleza pia kuwa wakati Serikali imedhamiria kuendelea na kuongeza fedha za bajeti kwa matumizi ya kununulia chakula kwa wagonjwa wanaolazwa katika hospitali nchini ameutaka uongozi wa hosptali hizo kuhakikisha kunakuwepo na uangalizi mzuri wa matumizi ya fedha hizo ili ziweze kuwafikia walengwa ipasavyo.

“Serikali tutaendelea kuongeza bajeti ya chakula kwa ajili wa wagonjwa lakini ni lazima viongozi wa hospitali wahakikishe kuwa fedha hizo zinatumika ipasavyo kuanzia manunuzi, upishi hadi kinavyowafikia wagonjwa” Dk. Shein alifafanua.

Aliongeza kuwa ni muhimu kwa sasa hospitali nchini ikiwemo ya Mnazi Mmoja kuajiri wataalamu wa lishe kwani kuwepo kwa wataalamu wa aina hiyo sio tu kutasaidia kupunguza gharama za chakula bali pia kuwapatia wagonjwa chakula wanchostahili kulingana na mahitaji ya afya zao.

Dk. Shein aliiagiza wizara hiyo kufanya utafiti wa matumizi ya tumbaku katika visiwa vya Unguja na Pemba ili kuona mwenendo wa utekelezaji wa Sheria ya Zanzibar ya Afya ya Jamii ya mwaka 2012 pamoja na Azimio la Shirika la Afya Ulimwenguni –WHO kuhusu matumizi ya tumbaku.

“utafiti huo uonyeshe mwenendo wa matumizi ya tumbaku na athari zake kwa kulinganisha Unguja na Pemba” Dk. Shein alisema na kusisitiza umuhimu wa Zanzibar kushiriki kikamilifu katika harakati za ulimwengu kupambana na matumizi ya tumbaku.

Aidha, Rais wa Zanzibar ameuagiza uongozi wa Wizara ya afya kutosita kufanya manunuzi ya dharura ya dawa au vifaa vya tiba pale inapotokezea haja ya kufanya hivyo ili kuokoa maisha ya wagonjwa badala ya kusubiri utaratibu mwingine ukiwemo wa kusubiri misaada.

Amesema mfumo wa biashara wa kisasa unarahisisha kufanya mambo mengi na kwa haraka, hivyo siyo vizuri kusubiri misaada kwa yale mambo ambayo yamo ndani ya uwezo wa Serikali.

Rais wa Zanzibar alirejea wito wake wa kuzitaka taasisi za umma ikiwemo wizara ya Afya kujenga utamaduni wa kulipia huduma za umeme na maji zinazotumika kwenye taasisi zao ili huduma hizo ziweze kuwa endelevu.

“Tunapodaiwa ni lazima tulipe hakuna lugha nyengine ya kuzungumza kwa kuwa hiyo ni biashara na kwamba Shirika la Umeme Zanzibar -ZECO lenyewe linanunua umeme kutoka TANESCO na lisipolipa tutakatiwa umeme na sote tutakosa huduma hiyo” alisisitiza Mhe Rais wa Zanzibar.

Awali akiwasilisha taarifa hiyo ya utekelezaji Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Dk. Mohamed Saleh Jidawi alieleza wizara hiyo kwa ujumla imeweza kutekeleza mengi ya majukumu yake katika kipindi husika kama yalivyoainishwa katika Mpangokazi wa Wizara hiyo pamoja na baadhi ya maagizo yaliyotolewa katika kikao kama hicho kilichofanyika mwezi Novemba 2013.

Mkutano huo ulihudhuriwa pia na Makamu wa Kwanza wa Rais Maalim Seif Sharif Hamad na Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi Dk. Abdulhamid Yahya Mzee.


0 comments:

Post a Comment