THE
UNITED REPUBLIC OF TANZANIA
DIRECTORATE
OF PRESIDENTIAL COMMUNICATIONS
Telephone: 255-22-2114512, 2116898
E-mail: ikulumawasiliano@yahoo.com
Fax:
255-22-2113425
|
PRESIDENT’S OFFICE,
THE STATE HOUSE,
P.O. BOX
9120,
DAR ES SALAAM.
Tanzania.
|
TAARIFA
KWA VYOMBO VYA HABARI
TAMKO LA
KATIBU MKUU KIONGOZI KWA VYOMBO VYA HABARI
KUHUSU
HATI YA MUUNGANO WA TANGANYIKA NA ZANZIBAR
IKULU, DAR
ES SALAAM, TAREHE 14 APRILI, 2014
__________________________________________________
Siku
12 zijazo tutasherehekea miaka 50 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, na
kuzaliwa kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Wamezaliwa watu ndani ya Muungano
huu na wengine wana wajukuu.
Inasikitisha
sana kuwa leo, miaka 50 baadaye ipo dhana potofu inayojengwa kuwa Muungano huu
si halali kwa vile hakuna Hati ya Muungano (Articles
of the Union).
Waasisi
wa Taifa letu ambao tarehe 22 Aprili, 1964 kule Zanzibar walitia saini Hati
hiyo, mbele ya mashuhuda, nao wameonekana kama walichokifanya kilikuwa kiini
macho, na kwa hiyo kwamba waliongoza Taifa jipya la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
kwa msingi wa kiini macho hicho kwa miaka yote hadi Mwenyezi Mungu alipowaita.
Mambo
yote mawili yametusononesha sana sisi Serikalini, na bila shaka yamewasononesha
wananchi wanaoipenda nchi yao, wanaowapenda Waasisi wa Taifa letu na kuuenzi
Muungano wao.
Madai
ya kuonyeshwa Hati ya Muungano yalianza siku nyingi lakini hatukuweza kuamini
hali itafikiwa ilipofikia, ambapo wapo watu wanathubutu kudai na kuapa kuwa
Hati hiyo haipo.
Ukweli
ni kuwa hati hiyo ipo, ilikuwepo siku zote. Hata hivyo, lazima tukubaliane kuwa
zipo Hati fulani ambazo ni kiini cha uwepo wetu kama Taifa huru, Jamhuri huru
na Muungano huru, ambazo tunazihifadhi kama mboni ya jicho. Hati hizo ni pamoja
na Hati ya Uhuru wa Tanganyika ya mwaka 1961, Hati ya Tanganyika kuwa Jamhuri
mwaka 1962, na Hati ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ya mwaka 1964. Hati
za aina hii zinahifadhiwa maeneo maalum ambayo ni salama ili zisipotee wala
kuharibika. Kwa kawaida hatuzitoi, tunazifungua ili kuzihifadhi kwa namna
yoyote ile.
Lakini sasa maneno yanakua mengi, tuhuma zimekuwa nyingi, dhihaka zimekuwa nyingi, kiasi cha wananchi kuanza kutiwa mashaka iwapo kweli Hati ya Muungano ipo au la.
Hivyo,
kwa maagizo na ridhaa ya Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania, ninaleta mbele yenu Hati ya Muungano wa Tanganyika na
Zanzibar iliyotiwa saini Zanzibar na waasisi wetu, Mwalimu Julius Kambarage
Nyerere na Mzee Abeid Aman Karume, ili muione na kuwahakikishia Watanzania kuwa
yanayosemwa kuwa hakuna Hati hiyo si kweli. Hati hiyo ipo tangu wakati huo,
imetunzwa vizuri na waliotutangulia, tumeirithi, na tutaendelea kuihifadhi.
Na, tukiombwa kufanya hivyo na Mwenyekiti wa Bunge Maalum nina uhakika Rais ataridhia ipelekwe huko ili kuondoa mjadala wa kama Hati ipo au la.
Isitoshe, tufanye utaratibu wa kuweka nakala kwenye Makumbusho ya Taifa ili kila atakayetaka kuiona katika miaka mingine 50 ijayo na kuzidi aione.
Mwisho, narejea kusema kuwa kwa upande wa Serikali tunasikitishwa na kufadhaishwa sana na tuhuma nzito kwamba labda waasisi wetu hawakuwa makini au walitufanyia kiini macho. Hatukutarajia wawepo Watanzania wenzetu, wafikie hapo.
Ni
jambo zito. Vile vile hatukutarajia kuwa Serikali itatuhumiwa kuwa haikuwa
makini kuhifadhi waliosaini waasisi wetu.
Matumaini
yetu ni kuwa baada ya leo tutaendelea na mambo ya msingi kwa mustakabali, umoja
na uimara wa Taifa letu badala ya kuchochea hisia kuwa Muungano wetu hauna
msingi imara wa kisheria.
Imetolewa
na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya
Rais,
Ikulu,
DAR
ES SALAAM.
14 Aprili, 2014
0 comments:
Post a Comment