Zaidi ya watu milioni 130 katika kanda ya Afrika Mashairki wanazungumza lugha ya Kiswahili ambacho ni lugha kuu katika kanda hiyo.
Hata hivyo bado Jumuiya ya Afrika Mashariki iliyo na nchi tano wanachama, haijatambua wala kuidhinisha matumizi ya lugha hiyo kama lugha rasmi ya kanda.
Lakini mwishoni mwa mwezi jana baadhi ya wabunge wa bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki, walipendekeza mkataba wa makubaliano ya Jumuiya hiyo ufanyiwe marekebisho ili lugha hiyo itambuliwe rasmi.
Lakini je, lugha hii ina umuhimu katika maendeleo na ustawi wa Jumuiya hiyo?
Mwandishi wetu Mark Muli anaripoti.
Ngabo Nkurunzinza ni raia wa Rwanda na mhadhiri wa chuo kikuu hapa jijni Nairobi, na amekuwa humu nchini kwa muda sasa, lakini alipowasili humu nchini kwa mara ya kwanza alikuwa na shida moja.
Sauti - Ngabo Nkurunzinza - Ilibidi nijifunze Kiswahili
"Wakati nilitoka Rwanda nilipofika hapa jijini Nairobi nilikuwa najua Kifaransa tu, nikapata ni vigumu kuwasiliana na watu ikabidi nianze kujifunza Kiswahili mimi mwenyewe."
Sasa kutoka na umuhimu wa lugha hii kwa mawasiliano bunge la Jumuiya ya Afrika masahariki limependekeza lugha ya Kiswahili, kuwa lugha rasmi ya Jumuiya.
Lakini kwake Timothy Kitui Wanyinyi ambaye ni msomi wa mambo ya ushirikiano wa Kimataifa, na pia mhadhiri katika vyuo mbali mbali humu nchini ni kwamba hatua hiyo, ingekuwa ndilo jukumu la kwanza kwa Jumuiya hiyo kutekeleza.
Sauti - Timothy Kitui Wanyonyi - Lugha ingekuwa ya kwanza
"Ningesema kwamba hilo linafaa kuwa lingekuwa jukumu la kwanza kwa Jumuiya hii.Sababu ikiwa haileti maana kuvunja mipaka kibiashara, kiusafiri na katika mambo mengine na tukose kuvunja mipaka kilugha kwa hivyo kurasmisha lugha ya Kiswahili katika Jumuiya ya Afrika Mashariki kwangu mimi kama msomi wa uhusiano wa Kimataifa naona ni kitu kimekuja katika wakati unaofaa na hata kwangu ni mpango ambao umechelewa na ninaunga hilo mkono."
Hata kabla ya pendekezo hilo kutolewa mataifa mawili ya Jumuiya hiyo ya Burundi na Uganda, ambayo hutumia lugha hiyo kwa uchache, yameanza harakati ya mafunzo ya lugha hiyo katika mashule na vyuo vyake.
Uganda tayari imekamilisha kuunda silabasi ya lugha hiyo katika shule zake, huku nchini Burundi lugha hiyo ikifunzwa katika shule na vyuo mbali mbali japo kwa uchache.
Lakini kwanza lugha ina umuhimu gani kwa jamii kijumla?
Joseph Musyoki ni mhadhiri katika chuo kikuu cha PECA, hapa nchini Kenya na anaeleza.
Sauti - Joseph Musyoki - Umuhimu wa Lugha.
"Ili watu waweze kuwasiliana lazima wawe na lugha moja ambayo wanaielewa na utapata kwamba kama hakuna lugha ambayo inaeleweka na watu katika hali ya mawasiliano kutakuwa na ugumu wa kuwasiliana.Lakini kama watu wana lugha moja ambayo wanaielewa vizuri mawasiliano yatakuwa rahisi sana kwa hivyo ni vizuri kuwa na lugha inayoeleweka sana na wengi."
Wengi wamesema lugha hii ikizingatiwa na kuwekwa rasmi itaweza kukuza Uchumi wa kanda hii na wananchi wake kupitia Biashara.
Reuben Sibaya ni raia wa Tanzania.
Sauti - Reuben Sabaya - Umuhimu wa Kiswahili
"Lugha ya Kiswahili itaweza kuunganisha jamii yote ya Afrika Mashariki, itaweza kutuunganisha kwa njia nyingi kama vile biashara, kama mimi unavyo niona hapa, kwa hivyo itakuwa rahisi kwa mwanaafrika mashariki wakati unatembea katika nchi tofauti kufanya biashara."
Naye Nkurunziza anasema lugha hii pia itachangia kumaliza migogoro, na vita zinazotokana na kutoelewana katika kanda na itawaleta pamoja wananchi wake.
Sauti - Ngabo Nkurunzinza - Italeta uwiano
"Lugha hii ikipitishwa na kuwa lugha rasmi itasaidia kanda hii kwa njia nyingi sana.Vitu kama vita za kikabila zitapungua sana.Watu watakuwa wakiketi pamoja kuzungumza na kuelewana na kwa hilo urafiki utaenea sana.Kwa hivyo itakuwa ni vyema kwa lugha hii kutumika katika Jumuiya hii kama Lugha rasmi."
Timothy Wanyonyi anaeleza pia lugha hii itainua pakubwa sekta ya elimu.
Sauti - Timothy Kitui Wanyonyi - Itasaidia pia katika elimu
"Itasaidia pia katika taaluma mbali mbali za kielimu, kuna wanafunzi huwa hawafanyi vyema katika masomo shuleni na sio eti kwamba hawaelewi lakini shida ni lugha inayotumiwa ndiyo shida.Kwa hivyo sidhani kwamba wanafunzi wangefeli sayansi jinsi wanavyifeli ingekuwa inafunzwa na lugha nyingine tofauti na kimombo."
Joseph Musyoki anasema lugha hii itakuwa ya maendeleo makubwa kwa kanda hii, kuliko lugha nyingine yoyote ile.
Sauti - Joseph Musyoki - Lugha uleta maendeleo
"Wakati tunakuza lugha ile lugha inaleta maendeleo, kwa mfano katika sekta ya uchapishaji, na pia muziki.Unapata wanamuziki wengi wakiimba kwa lugha ya Kiswahili huwa wanafanya vyema zaidi kuliko lugha zao za kitamaduni."
Ni katika njia nyingine ipi lugha hii itakuwa ya muhimu?
Sauti - Timothy Kitui Wanyonyi – Kitambulisho
"Hiyo itatusaidia kuwa na kitambulisho kama wana wa Jumuiya hii.Na hilo ni jambo la msingi sana."
Hata hivyo anaonya dhidi ya kushikilia lugha hii na kusahahu lugha zingine muhimu, kwa maendeleo ya kanda katika ramani ya Dunia.
Sauti - Timothy Kitui Wanyonyi - Hata hivyo tusisahahu
"Lakini sio kwamba tunafunga milango.Kuna lugha zingine za kigeni ambazo zinakuja kama vile Kichina, Kifaransa na kadhalika lakini lazima tuwe na kitambulisho chetu."
Kwa ujumla lugha ya Kiswahili barani Afrika utumika katika mataifa 12 huku ikiwa rasmi katika mataifa matatu ya Kenya, Rwanda na Tanzania, na kwa wengi wanaona na kutaja kuwa lugha hii pia inaweza kuwa lugha rasmi ya mwafrika.
Lakini ikiwa hilo litafikiwa itategemea na ushawishi na mapenzi ya serikali za Kiafrika.
0 comments:
Post a Comment