Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amesema Wajumbe wa Baraza la
Wawakilishi wana jukumu kubwa la kuisimamia na kuishauri Serikali Kuu ili
kuhakikisha matatizo na kero zinazowakabili Wananchi katika maeneo mbali mbali
nchini zinatatuliwa kwa ufanisi na mafanikio makubwa.
Amesema
Wawakilishi pia wanapaswa kuhakikisha kuwa Serikali inatoa mchango wake
kikamilifu katika kuyafanya maisha ya Wananchi wote kuwa bora zaidi kwa kutumia
nguvu kazi na rasilmali zilizopo hapa Nchini.
Akitoa
hoja ya kuahirisha Mkutano wa kwanza wa Baraza la Tisa la Wawakilishi Zanzibar
huko katika Ukumbi wa Baraza hilo Mbweni nje kidogo ya Mji wa Zanzibar Balozi
Seif amesema Serikali ina matarajio ya kupata Taarifa na ushauri kutoka kwa
Wawakilishi hao juu ya maeneo yatakayohitaji kupewa msukumo ili kuongeza kasi
ya Maendeleo.
Amesema
heshima kubwa waliyotoa Wananchi katika kuwachaguwaWawakilishi hao kuwa Wajumbe
wa Baraza la Wawakilishi iwe macho na masikio yao katika mategemeo ya kusaidiwa
kutatua changamoto zaombali mbali za maendeleo zinazowakabili kila siku.
“
Sisi ndio masikio na macho ya Wananchi. Wametupa heshima kubwa kwa kutuchagua
kuwa wajumbe wa Baraza hili wakiwa na mategemeo
makubwa tutawasaidia kutatua
changamoto tofauti za maendeleo zinazowakabili ”. Amesema Balozi Seif.
Amewaomba
waheshimiwa Wawakilishi kwa vile uchaguzi umekwisha warudi Majimboni mwao ili kushirikiane
na Wananchi wao katika kuelekeza nguvu zao kwenye harakati za maendeleo
sambamba na kudumisha amani na utulivu wa Visiwa hivi.
Amesema
Serikali itaendelea kusimamia suala la
amani na utulivu kwa nguvu zote ili kutekeleza mipango ya kujiletea maendeleo
zaidi ya Kiuchumi, Kijamii na Kisiasa.
Balozi Seif amesema hakuna haja ya
kukumbushana mambo yaliyopita licha ya Serikali kutambua wapo baadhi ya Watu wakorofi
wanaojihusisha na vitendo vya kuhatarisha amani ya Nchi iliyopo kwa sasa.
Amefahamisha
kuwa wakorofi hao walijihusisha na utegeji wa miripuko inayosadikiwa kuwa
mabomu na kuchoma moto mashamba ya mikarafuu, nyumba za baadhi ya wananchi
pamoja na maskani za Chama cha Mapinduzi.
Amesema
vyombo vya dola vinaendelea na hatua ya
uchunguzi wa matukio hayo na baadaye kuchukuwa hatua kwa mujibu wa
sheria na kuonya kwamba hakutakuwa na mtu atakayepona kuchukuliwa hatua kali za
kisheria iwapo atabainika kutishia amani na utuliovu wa Taifa.
Akizungumzia suala la uwajibikaji katika Taasisi za Umma Makamu wa Pili wa Rais
wa Zanzibar Balozi Seif amewaomba
Watendaji wote wa Serikali
watakaoteuliwa hapo baadae wakubali kwa moyo wao mkunjufu kuwatumikia
Wananchi bila ya kujali itikadi zao za kisiasa, jinsia au Dini.
Balozi
Seif amesema Serikali muda wote imekuwa ikihimiza uwajibikaji sambamba na
usimamizi mzuri wa fedha na rasilmali nyengine za umma katika ngazi zote.
Ameonya
kwamba zipo Idara na Taasisi za Serikali zilizooza sana na kulalamikiwa na Wananchi kwa sababu ya kutowajibika kwa
watendaji wa Taasisi hizo. Hivyo amehidi kumsaidia Rais katika kuyatumbua
majipu yatakayojitokeza.
“
Nawaomba watendaji watakaoteuliwa wasikae maofisini tu, bali wazitemnbelee
taasisi zilizo nchini yao ili waone uwajibikaji wa Taasisi hizo. Na mimi
naahidi kumsaidia Mheshimiwa Rais katika kuyatumbua majipu yatakayojitokeza ”.
Alisema Balozi Seif.
Akigusia
tabia ya baadhi ya wafanyabiashara kuuza bidhaa
zao katika mfumo wa ubaguzi kwa sababu za itikadi za Kisiasa Balozi
Seif ameonya kwamba jambo hilo sio zuri
na ingefaa likaachwa mara moja.
Amesema
inasikitisha na mambo yanayotokea katika baadhi ya maeneo Kisiwani Pemba ambako
baadhi ya wafanyabiashara wameanzisha mtindo wa kuwanyima Wananchi wenzao
kuwauzia bidhaa kwa sababu za tofauti za kisiasa.
Balozi
Seif ameeleza kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inalifuatilia kwa karibu
suala hilo na haitasita kumchukulia hatua kali za kisheria mfanyabiashara yeyote
atakayebainika kuendeleza jambo hilo ikiwa ni pamoja na kumfutia mara moja leseni yake ya biashara.
Akigusia
migogoro ya ardhi iliyoleta changamoto kubwa kwa Serikali katika kipindi
kilichopita Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amesema kadhia hiyo kwa kiasi
kikubwa imesababishwa na baadhi ya Viongozi kwa sababu ya tamaa.
Balozi
Seif amesema hata baadhi ya wananchi wamekuwa wakiendelea na ujenzi holela wa
nyumba za kudumu bila ya kibali na wakati mwengine katika maeneo yasiyoruhusiwa
kama vile sehemu za vianzio vya maji pamoja na maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya
ujenzi wa miji ya kisasa.
Amewatanabahisha
watu wote waliojenga katika maeneo hayo kuacha kufanya hivyo mara moja sambamba
na Viongozi wenye tamaa ya fedha au kujilimbikizia maji wajisafishe kabla
mkondo wa sheria haujawakumba.
Mapema
ndani ya kipindi cha siku mbili cha
Mkutano huo wa Baraza la Wawakilishi
Wajumbe wa Baraza la hilo walipata fursa ya kuijadili Hotuba ya Rais wa
Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dr. Ali Mohammed Shein aliyoitoa
mapema wiki hii wakati akilizindua rasmi Baraza hilo.
Pamoja
na mambo mengine Wajumbe kadhaa wa Baraza hilo walielezea umuhimu wa Wananchi
kwa kushirikiana na viongozi wao Majimboni kuelekeza nguvu zao katika ujenzi wa
Taifa ili kuisimamia ipasavyo Ilani ya
Chama kilichopata ridhaa ya kuongoza Dola katika Kipindi cha miaka mitano ijayo
ambacho ni CCM.
Mkutano
wa kwanza wa Baraza la Tisa la Wawakilishi Zanzibar umeahirishwa katika Ukumbi
wa Baraza hilo Mweni hadi asubuhi ya Jumatano ya Tarehe 18 Mei 2016.
0 comments:
Post a Comment