March 16, 2016

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga amesema ulinzi umeimarishwa na kuwataka wananchi visiwani humo kujitokeza kwa wingi kumchagua viongozi wanaompenda siku ya uchaguzi huo Machi 20, 2016 na watarejea nyumbani kwao salama mara baada ya kumaliza kupiga kura.
Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kumaliza mazungumzo na Maafisa Waandamizi wa Jeshi la Polisi Makao Makuu ya Polisi Zanzibar na baadaye kuzungumza na Wakuu wa vyombo vya Ulinzi na Usalama, Waziri Kitwanga alisisitiza kuwa, vyombo vya ulinzi na usalama vimejiandaa vizuri na wananchi waondoe shaka kwani hawatakubali vurugu ya aina yoyote itokee. 
“Jitokezeni kupiga kura siku ya uchaguzi kwani ni haki yenu, nawahakikishia usalama upo na wa hali ya juu, asijitokeze mtu yeyote akawatisha kutokuja kupiga kura, tumejipanga vizuri na lengo letu kubwa kabisa ni kuwalinda wananchi,” alisema Kitwanga.

Hata hivyo Waziri Kitwanga alisema hakuna mwananchi yeyote anayehama kwa kuogopa vurugu siku ya uchaguzi bali watu wanasafiri kwasababu mbalimbali ikiwemo hiki ni kipindi cha maandalizi ya Sikukuu ya Pasaka, baadhi ya wananchi wanaenda kula sikukuu maeneo mbalimbali nchini na wengine wanasafiri kutokana na majukumu mbalimbali na sio wamekuwa wakimbizi wakikimbia sehemu zao kama inavyoenezwa.
“Acheni kusikia habari za mitaani amani ipo, jitokezi kupiga kura na hii habari mnayosikia eti watu wameanza kuyakimbia makazi yao ni uzushi tu, hakuna kitu kama hicho, wananchi wanaendelea na shughuli zako kama kawaida na vyombo vya ulinzi vimejipanga kwa ajili ya kulinda usalama wa raia na mali zao,” alisema Kitwanga.
Waziri Kitwanga amewasili Zanzibar leo kwa ajili ya ziara ya kikazi ya kuimarisha usalama zaidi visiwani humo pamoja na kujua mikakati iliyowekwa na vyombo vya ulinzi na usalama kuhusu usimamizi wa uchaguzi huo.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga (kushoto) akisalimiana na Brigedi Kamanda wa 101 KV Zanzibar, Brigadia Jenerali, Cylir Mhaiki, kabla ya kufanya mazungumzo na Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama mjini Zanzibar. Kulia ni Kamishna wa Jeshi la Zimamoto na Uokozi, Zanzibar, Ali Abdalla Maalimmosi. Waziri Kitwanga yupo Zanzibar kwa kwa ziara ya kikazi ya kuangalia hali ya uimarishaji wa usalama visiwani humo.


0 comments:

Post a Comment