March 15, 2016


Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amewaagiza watendaji wa Wizara ya Afya  hasa Madaktari na wauguzi kuhakikisha kwamba dhima waliokabidhiwa na jamii katika kuwahudumia  Wananchi Kiafya wanaitekeleza kwa moyo na imani kama walivyokula kiapo.
Balozi Seif Ali Iddi  alieleza hayo wakati alipofanya ziara ya ghafla katika Hospitali ya Rufaa ya chake chake Kisiwani Pemba kuangalia hali ya uwajibikaji pamoja na kukutana na Uongozi wa Wizara ya Afya uliongozwa na  Afisa Mdhamini wake Dr.Mkasha Hijja Mkasha.
Ziara ya ghafla ya Balozi Seif imekuja kufuatia tetezi kwamba zipo dawa nyingi zilizoharibika huku wagonjwa wanaokwenda kupata huduma  kwenye Hospitali hiyo wakilalamika kulazimika kununua  baadhi ya dawa hizo pamoja na ukosefu wa Tanuri la Kuchomea  lililokosekana tokea mwaka.
Balozi Seif alisema Madaktari na wauguzi wanapaswa kutambua kwamba wao ndio dhamana wa kulinda afya za Wananchi katika maeneo yao, kinyume cha wajibu huo watarajie kujenga chuki na uhasama kati yao na Wananchi hao hasa wagonjwa wanaopelekwa kuwahudumia.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwatahadharisha baadhi ya Madaktari na wauguzi wenye hulka ya kunyanyasa wagonjwa  kwa kisingizio cha itikadi za Kisiasa waelewe kwamba tabia hiyo hawaikomoi Serikali bali wanawatesa Wananchi hasa wagonjwa wasiokuwa na hatia yoyote.
Akizungumzia tatizo laTanuri la kuchomea taka taka za Hospitali hiyo ya Chake chake  Pemba Balozi Seif aliulaumu Uongozi wa Wizara ya Afya kwa kushindwa kukamilisha ujenzi wa Tanuri hilo kwa miaka Mitano sasa.
Alisema hali hiyo haileti sura nzuri katika dhana nzima ya uwajibikaji kwa watendaji hao jambo ambalo Serikali Kuu italazimika kulichukulia hatua za haraka tatizo hilo lenye kuleta hali ya wasi wasi wa afya za Wananchi wanaoishi karibu na maeneo hayo.
Balozi Seif aliuonywa Uongozi wa Wizara ya Afya kwamba kama utashindwa uwezo wa kutoa shilingi Milioni 3,500,000/-  hata kwenye O.C  za mwezi za Wizara hiyo kujenga Tanuri jengine basi ataamua kutoa fedha yeye mwenyewe kuondosha kadhia hiyo inayoleta kero na wasi wasi kwa wakaazi wa maeneo ya Mji huo.
Mapema Mkuu wa Wilaya ya Chake Chake Bibi Hanuna Ibrahim Masoud alisema Ofisi yake imekuwa ikipokea malalamiko  mengi kutoka kwa Wananchi wa maeneo ya Mji wa Chake chake kuhusu kutapakaa kwa taka taka zinazozalishwa na Hospitali hiyo zikikosa hifadhi ya kudumu.
Bibi Hanun alisema Wananchi hao wamekuwa wakishuhudia baadhi yawanyama kama Mbwa na Paka wakiranda na taka taka hizo ambazo nyengine ni za hatari na zinaweza kusababisha kutapakaa kwa maradhi ya kuambukiza.
Balozi Seif akikagua baadhi ya wagonjwa kwenye wodi tofauti za 
Hospitali ya Chake chake Pemba  akiongozwa na 
Muuguzi wa Wodi ya Akina mama bi Hassanat Abdalla.


Balozi Seif akikagua Tanuri la kuchomea taka taka za Hospitali ya 
Chake chake ambalo limeshindwa kutoa huduma tokea 
lilipojengwa kwa miaka mitano sasa

0 comments:

Post a Comment