March 15, 2016

Watu wasiojulikana wamerusha kifaa kinachosadikiwa kuwa ni bomu katika nyumba ya Kamishna wa polisi Zanzibar  Hamdani Omar Makame kwake usiku wa kuamkia jana na kuathiri sehemu ya paa na dari la nyumba hiyo iliyopo katika mitaa ya Bububu Kijichi, mkoa wa Mjini Magharibi, Unguja.
Kamishna hamdani amethibitisha kutokea kwa mripuko huo wa bomu alioueleza kuwa ni sehemu ya mlolongo wa matukio ya kihalifu yanayotokea Zanzibar, lilitokea majira ya saa 5 usiku bila ya kuathiri maisha na kueleza kuwa uchunguzi kuhusiana na tukio hilo umeanza.
Kiongozi huyo mkuu wa jeshi la polisi Zanzibar, aliitisha mkutano na waandishi wa habari katika makao makuu ya jeshi hilo visiwani humu, kuzungumzia hali ya ulinzi na usalama visiwani Zanzibar akirejelea matukio mbali mbali ya kihalifu Zanzibar yaliyotokea toka kufutwa kwa uchaguzi mkuu wa Zanzibar Oktoba 28, mwaka jana.
Matukio aliyoyarejea ni pamoja na mripuko wa bomu uliotokea katika maskani CCM ya Kisonge, kuchomwa moto nyumba na majengo taasisi za umma na kisiasa, kisiwani Pemba na uimarishawaji wa hali ya ulinzi na usalama kuelekea katika uchaguzi mkuu wa marudio utakaofanyika baadae wiki hii.
“Katika kipindi hiki, kumetokea mambo mengi yenye mnasaba na harakati za kisiasa na uchaguziujao, hivyo jeshi la polisi kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama tumeamua kuchukua hatua madhubuti ili kuhakikisha tunadhibiti vitendo vyote vya kihalifu bila ya kujali nani anaefanya au nani anaewatuma”, alisema Kamishna Hamdani bila ya kwenda mbali zaidi kuhusu mripuko wa nyumbani kwake kwa kile alichodai kuwa hana taarifa za kutosha.
Mripuko wa Bomu la maskani ya CCM Kisonge
Akizungumzia mripuko wa kisonge uliotokea Machi 3 mwaka huu na kuathiri sehemu ya ofisi hiyo na baadhi ya nyumba za karibu na eneo la tukio, kamishna Hamdani alisema uchunguzi wa awali umebaini kuwepo kwa uhusiano kati ya bomu hilo na mengine yaliloripuka awali katika maeneo tofauti.
“Uchunguzi wa kisanyansi wa tukio hilo bado unaendelea ikiwa ni pamoja na kuwasaka wahalifu wote waliofanya kitendo hicho na tunaahidi katika kipindi kifupi kijacho watuhumiwa hao watatiwa mbaroni na kushughulikiwa kwa mujibu wa sheria”, alisema kamishna huyo na kuwataka wananchi kutokuwa na hofu ya wingi wa askari wa vikosi mbali mbali waliopo nchini.
Uchomaji wa nyumba Moto wa Pemba
Akizungumzia matukio hayo ambayo yalitokea jumamosi iliyopita ambapo nyumba 11 za makaazi ya wananchi, maskani 3 za CCM na kituo cha afya kimoja vilichomwa moto na watu wasiojulikana katika mkuoa wa kaskazini Pemba, Hamdani alisema jeshi lake limechukua hatua na kwamba hadi sasa linawashikilia watu 31 kwa mahojiano.
Akijibu hoja kuwa kutokana na tukio hilo polisi wamekuwa wakichukua hatua kali zaidi zinazowafanya baadhi ya wananchi kukimbia makaazi yao, alisema tuhuma hizo sio kweli na kwamba watu wanaoshikiliwa wanatokana na taarifa za kiintelijensia uliofuatiwa na msako mkali wa jeshi hilo.
Mapema juzi chama cha wananchi cuf kupitia kwa kaimu mkurugenzi wa habari, uenezi na mawasiliano kwa umma Hamad Masoud Hamad alisema katika kulishughulikia jambo hilo polisi wanatumia nguvu zaidi kiasi cha kukiuka misngi ya haki za binadamu jambo ambalo kamishna hamdani alilikanusha na kuwataka viongozi wa kisiasa kuacha kuchochea uwepo wa matukio ya kihalifu.
“Polisi inafanya kazi kutokana na taarifa inazokuwa nazo, hivyo kama kuna mtu anahusika na taarifa inayotufikia hatutasita kumshughulikia au kuchukua hatua dhidi yake kwa kuwa huo ndio wajibu wa msingi wa majeshi yote, sasa kama mtu hayataki haya asiwachochee wengine kufanya uhalifu kwa kisingizio cha siasa”, alisema.
Hali ya ulinzi na usalama
Akizungumzia hatua ya kuimarishwa kwa hali ya ulinzi na usalama katika maeneo mbali mbali ya Unguja na Pemba kuelekea katika kipindi hiki cha uchaguzi, kamishna hamdani alisema hali hiyo imelenga katika kuwahakikishia usalama wananchi ili waweze kutumia haki yao ya kidemokrasia na kuwataka kujitokeza kwa wingi siku ya kupiga kura.
“Napenda kuwahakikishia wananchi kuwa pamoja na kuwepo kwa viashiria vingi vya kihalifu, bado ulinzi utakuwa wa kutosha kabla, wakati na baada ya uchaguzi kwani tumeamua kuongeza nguvu ya ulinzi katika maeneo yote yanayotiliwa shaka ya kupangwa vitendo vya kihalifu”, alisema.
Kuhusu matumizi ya wanajeshi katika baadhi ya maeneo ya umma, Kamishna Hamdani alisema hilo ni jambo la kawaida kwa kuwa majeshi yote yana lengo moja la kulinda katiba, mipaka ya nchi na usalama wa raia na  mali zao, na kwamba hatua hiyo inalenga katika kuongeza idadi ya askari polisi katika doria na ulinzi wa mitaani.
"Majeshi katika nchi yeyote yana wajibu mmoja wa kulinda mipaka ya nchi na katiba yake, usalama wa raia na mali zao sasa kuna shida gani polisi wanapokabidhi baadhi ya majukumu kwa askari wa vikosi vyengine? hili ni jambo la kawaida kwa raia wema ila kwa wale wenye akili za kihalifu ni lazima walilalamikie kwani linawanyima fursa ya kutekeleza uhalifu wao", alisema kamishna Hamdani. 

Habari za kutokea mripuko nyumbani kwa kiongozi huyo wa jeshi la polisi Zanzibar zilianza kuzagaa mapema asubuhi ya jana huku askari polisi waliokuwa katika mavazi maalum kwa kushirikiana na vikosi vya serikali ya mapinduzi Zanzibar vikionekana kuimarisha ulinzi katika maeneo mbali mbali za mji wa Zanzibar huku kamishna huyo akiapa kuwashughulikia wale wote watakaobainika kufanya uhalifu huo na mwengine uliotokea kabla.


0 comments:

Post a Comment