Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
inaendelea na jitihada kuongeza idadi ya Wanawake katika vyuo na Taasisi ya
Elimu ya juu Nchini ili kiwango cha wanawake wenye elimu ya juu kikue
kila mwaka hasa katika elimu ya sayansi na ufundi.
Ongezeko hilo litakwenda
sambamba na kipaumbele cha kuwapatia mokopo ya elimu ya juu pamoja nakuanzishwa
program mbali mbali za kuwainua kielimu watoto wa kike hapa Nchini.
Makamu wa Pili wa Rais wa
Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema hayo wakati wa maadhimisho ya siku ya
Wanawake Dunia zinazofikia kilele chake kila ifikapo Tarehe 8 Mwezi Machi ya
kila Mwaka ambazo zimefanyika katika viwanja vya Kituo cha Simulizi Asili,
Tamaduni na lugha za Afrika { Eacrotanal } Mjini Zanzibar.
Balozi Seif alisema
ni ukweli usiofichika kwamba wanawake kutokana na umakini na umahiri
mkubwa walionao ni dhahiri kwamba wakipatiwa fursa na haki zao kikamilifu
ikiwemo elimu wanaweza kuleta mabadiliko makubwa ya kiuchumi na maendeleo ya
Taifa.
Alisema wanawake
wanaokadiriwa kufikia asilimia 51.6 % ya watu wote wa Zanzibar kwa mujibu
wa sensa ya watu ya mwaka 2012 wanawake ndio wanaotunza
na kuziendeleza familia, lakini wengi wao hawana uwezo wa kutosha wa
kuzihudumia familia zao.
Balozi Seif alitoa wito
kwa Taasisi zote zinazoshughulikia masuala ya uwezeshaji wananchi kiuchumi
kuwasimamia vyema wanawake ili kuwajengea uwezo utakaosaidia akinamama
hao kubeba jukumu lao la kuhudumia familia, lakini pia kuleta maendeleo
ya Taifa kwa jumla.
Alisisitiza umuhimu wa
changamoto ya umiliki wa rasilmali unaowakumba wanawake wengi kutafutiwa
ufumbuzi wa kudumu ili waweze kuwa na uhakika kwa kuziendesha familia zao
zinazowalazimu.
Alisema uzoefu unaonyesha
wazi kwamba wanawake walio wengi hawapati fursa ya umiliki wa
rasilmali zao kutokana na mfumo dume uliojengeka ndani ya jamii ukiwemo ule wa
uelewa mdogo wa wanawake wa kutambua haki zao na kuzifuatilia.
“ Suala ya umiliki mdogo
wa rasilmali kwa wanawake ambayo ndio nyenzo muhimu ya kujikomboa kimaisha
ni miongoni mwa changamoto zinazozorotesha maendeleo yao katika Nyanja
zote ”. Alisema Balozi Seif.
Makamu wa Pili wa Rais wa
Zanzibar alieleza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaendelea kuchukuwa
juhudi za kubuni mbinu, mikakati na kuandaa fursa mbali mbali za kuwawezesha wanawake
kiuchumi.
Alisema zipo Taasisi
zilizoundwa na kuanzishwa zikijikita katika kuhamasisha na
kuwajengea uwezo wanawake katika nyanja mbali mbali ikiwemo
ujasiriamali, uongozi, umiliki wa rasilmali ndogo na kubwa katika jamii
lengo likiwa ni kuwawezesha wanawake kuthubutu kumiliki rasilmali
zilizoizunguuka Jamii.
Akizungumzia tatizo la
udhalilishaji wa kijinsia unaowakumba zaidi wanawake na Watoto Balozi
Seif Serikali Kuu imedhamiria kupambana na kadhia hiyo ya
udhalilishaji inayolitia aibu Taifa na kufikia hatua ya kuanzisha kampeni kubwa
ya kupambana na maovu hayo karibu mwaka mmoja uliopita.
Balozi Seif alieleza kuwa
upo udhaifu unaojitokeza wakati wa mapambano dhidi ya udhalilishaji ambao
iwapo Viongozi, watendaji wa Taasisi zinazosimamia sheria pamoja na
Wananchi hawakushirikiana pamoja, majambazi wa matendo hayo
wataendelea kutamba na jamii itafikia hatua ya kudhania kama hakuna Serikali.
Alionya kwamba tabia ya
kufichiana vitendo vya udhalilishaji pamoja na kusuluhisha makosa hayo
inayofanywa na baadhi wabakaji ndani ya familia na mwanya wa
kupoteza vielelezo unakosesha ushahidi uliokamilika wa kuwatia hatiani
madhalimu wa maovu hayo.
Alifahamisha kwamba
ushirikiano wa pamoja kati ya taasisi zote na jamii kwa jumla ndio
utakaochangia kumaliza tatizo hilo la udhalilishaji wa kijinsia wa wanawake na
watoto hapa Zanzibar na kulirejeshea heshima yake ya Kihistoria Taifa hili.
Katika risala yao
wanawake hao iliyosomwa na Bibi Hadia Mohammed Ranadhan alisema wanawake Nchini
hawaridhiki na utendaji wa watumishi wa Mahakama, Polisi na Ofisi ya
Mkurugenzi wa Mashataka ambao umekuwa ukiwakosesha amani na furaha ya maisha.
Bibi Hadia alisema
usalama wa wanawake na watoto hivi sasa uko mashakani kutokana na kukithiri kwa
vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia unaendelea kufanywa na baadhi ya
watu Mitaani bila ya kuwa na hofu yoyote.
Alisema tabia ya waovu
hai imezidi kupanda batra kutokana na maamuzi ya watumishi wa taasisi
hizo kushindwa kutoa maamuzi yanayoleta faraja kwa watoto na wanawake waliodhalilishwa
katika maeneo mbali mbali hapa nchini.
Wakitoa salamu kwenye
kilele cha maadhimisho hayo ya siku ya wanawake Duniani Mwakilishi wa Shirika
la Umoja wa Mataifa la Idadi ya watu {UNFPA
}Dr.Natalia Kamem, Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Wanawake { UN
WOMEN } Lucy Tesha pamoja na Yule wa Shirika la kuhudumia Watoto { Save
the Children } Bwana Rashid Mohammed Hashim wameahidi kuendelea kuiunga mkono
Zanzibar katika harakati zake za kuwajengea uwezo Wanawake.
Wawakilishi hao walisema
haki ya kila mtu haitegemei jinsia yake bali ni uwezo wake katika kuihudumia
jamii iliyomzunguuka na kinachohitajika kwa Mataifa na Taasisi za Kijamii ni
kuhakikisha zinatoa huduma sawa hasa zile za elimu kwa watu wote na kuacha
tabia ya kiuendeleza mfumo dume uliozoeleka.
Walisema ushiriki wa
wanawake katika maeneo ya uzalishaji, ajira pamoja na kazi za ujasiriamali ndio
njia pekee itakayoifanya dunia inaendelea kuwa na amani na utulivu.
Katika maadhimisho hayo
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alikabidhi Mikopo yenye
Thamani ya shilingi Milioni 31,125,000/- kwa vikundi 13 vya ujasiriamali vya
wanawake kutoka Mikoa yote ya Unguja.
Vikundi hivyo ni pamoja
na Kijicho cha Chura kutoka Mkele, Hima Hima Gulioni, Hatuyumbi Sebleni, Hakuna
Kulala Group Sogea, Nia Njema Kidimni,Wasafi Group, Mola Tubariki Tazari,
Heri Tufanikiwe Kidombo, Gamba Mpya, Nungwi Imara, Kidimni Cooperative,
Tuaminiane Kimebe Samaki pamoja na Muungu yupo cha Welezo.
Mapema Makamu wa
Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alipata fursa ya kukagua maonyesho ya
wajasiriamali wanawake kutoka vikundi tofauti vya miradi ya uzalishaji
vya Wilaya za Unguja.
Balozi Seif alionyesha
kuridhika na kazi kubwa inayotekelezwa na akina mama hao katika suala zima la
kujiletea maendeleo yao kwa kupiga vita ukali wa maisha pamoja na kupunguza
umaskini.
Ujumbe wa mwaka huu wa
siku ya wanawake Duniani unasema “ Hakikisha usawa wa kijinsia kwa kuchukuwa
hatua madhubuti ”. Ujumbe unaofanyiwa kazi na Mataifa wanachama ya Umoja wa
Mataifa kwa mujibu wa mazingira halisi ya Nchi husika.
Kwa upande wa Zanzibar,
wanawake na washirika wake wameamua kuadhimisha siku hii ya wanawake Duniani
kwa kuhimiza suala la uwezeshaji wa wanawake kiuchumi kwa kupitia Ujumbe
unaosema. “ Wanawake ni wenza katika kukuza uchumi. Toa fursa sawa
wamiliki rasilmali ”.
Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Wanawake {UN
WOMEN}
Lucy Tesha akitoa
salamu kwenye maadhimisho ya siku ya wanawake Duniani
hapo Eacrotanal.
Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia
idadi ya watoto
{UNFPA} Dr. Dr.Natalia Kamem akitoa salamu kwenye maadhimisho
ya
siku ya wanawake duniani hapo Eacrotanal.
0 comments:
Post a Comment