Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, imeikabidhi Wizara
ya Afya vifaa vya maabara vyenye uwezo wa kubainisha dawa za kulevya.
Akikabidhi vifaa hivyo kwa Naibu Katibu wa Wizara ya Afya, Katibu
Mkuu Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Dkt. Omar Dadi Shajak, amesema kuna
umuhimu wa kuvitunza na kuvitumia vifaa hivyo kwa njia zilizo sahihi, ili
viweze kuleta tija katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya nchini.
Ametoa wito kwa jamii hasa wadau wakuu wanaohusika na mapambano
dhidi ya dawa za kulevya kufanya kazi kwa ushirikiano ili kuhakikisha kuwa
mapambano hayo yanafanikiwa.
Amesema Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais kupitia Tume ya Kuratibu
na Udhibiti wa Dawa za Kulevya Zanzibar, itaendelea kushirikiana na wadau wa
maendeleo ili kusaidia upatikanaji wa vifaa vya kisasa katika kufanikisha
mapambano hayo.
Amelishukuru Shirika la Umoja wa Mataifa la kupambana na dawa za
kulevya na uhalifu duniani (UN ODC) kwa kutoa vifaa hivyo vya dawa, na kuwaomba
washirika wengine wa maendeleo kusaidia juhudi hizo.
Mapema akipokea vifaa hivyo katika hafla iliyofanyika Ofisi ya
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Migombani, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya
Afya Bi. Halima Maulid Salum, ameishukuru Ofisi hiyo kwa jitihada zake
inazochukua katika kukabiliana na dawa za kulevya, na kuahidi kuvitumia vifaa
hivyo kwa uangalifu mkubwa.
Nae Mkemia Mkuu wa Serikali Zanzibar Dkt. Slim Rashid Juma,
amesema vifaa hivyo vitasaidia na kurahisisha uchunguzi wa dawa za kulevya, na
kuweza kutofautisha kwa haraka baina ya dawa hizo na kemikali.
Amesema matarajio ya maabara yao ni kuwa na vifaa vya kisasa kwa
ajili ya kurahisisha na kuwezesha kufanya uchunguzi wa aina zote za dawa za
kulevya, kwa lengo la kuondosha usumbufu wa kusafirisha sampuli kwenda Tanzania
Bara.
0 comments:
Post a Comment