Mabalozi wa nchi zinazounda Umoja wa Ulaya (EU) wameeleza
kusikitishwa na kitendo cha Tume ya Uchaguzi (ZEC) kutangaza tarehe ya marudui
ya Uchaguzi wakati mazungumzo ya kutatua mgogoro yakiendelea na kumtaka Rais
John Magufuli kutumia nafasi yake ya uongozi kutatua mtanziko wa kisiasa
visiwani Zanzibar.
Taarifa ya pamoja iliyotumwa kwa vyombo vya habari na
mabalozi hao jana, pia inamtaka Rais Magufuli kuendeleza wito wake wa kuzitaka
pande zote zitafute suluhu kwa amani.
Tamko hilo limetolewa siku saba baada ya mwenyekiti wa ZEC,
Jecha Salum Jecha kutangaza kuwa uchaguzi wa rais wa Zanzibar, wawakilishi na
madiwani utarudiwa Jumapili ya Machi 20, lakini siku tano baadaye CUF ilitoa
tamko la kutoshiriki uchaguzi huo wa marudio.
Kutokana na sakata hilo, mabalozi hao wamelaani kitendo
hicho wakisema kurudia uchaguzi kwa kigezo kuwa utaratibu ulikiuka, kinawatia
wasiwasi kwa kuwa tume hiyo haikutoa ushahidi wa ukiukwaji huo.
Mabalozi hao wamesema katika tamko lao kuwa ZEC imerudia
kauli yake ya kuwa uchaguzi ulikiuka taratibu licha ya waangalizi kutoka EU,
Jumuiya za Afrika Mashariki, Sadc Marekani na Jumuiya ya Madola kufanya
tathmini na kujiridhisha kuwa ulikuwa huru na haki.
“Tunasikitika kuwa ZEC imetangaza tena kuwa uchaguzi
utarudiwa Zanzibar, wakati mazungumzo baina ya pande mbili yanaendelea. Kwa
manufaa ya Watanzania wote, tunasisitiza kuwa hali ya kisiasa ya visiwani humo
ni bora ikatatuliwa kwa pande mbili kukubaliana,”inasema taarifa hiyo.
Taarifa hiyo iliyotumwa kwa ushirikiano wa mabalozi wa
Uholanzi, Norway, Hispania, Italia, Ujerumani, Finland, Ufaransa, Sweden,
Uswisi, Uingereza, Ireland na Marekani inasisitiza kuwa kitendo cha upande
mmoja kuamua kurudia uchaguzi, kinaweza kuzidisha hofu na taharuki miongoni mwa
Wazanzibari.
“Tunawaomba Wazanzibari kuwa watulivu na wavumilivu nyakati
hizi na tunazitaka pande zote mbili na washirika wao kuendelea kufanya kazi
pamoja ili wapate suluhisho la amani,” ilisema taarifa hiyo.
Pia inasema ili uchaguzi uwe wa kuaminika, mchakato wake
hauna budi kuziwakilisha pande zote na kuwa huru na wa haki.
Hata hivyo, mabalozi hao wamesema kulingana na mazingira ya
Zanzibar kwa sasa, itakuwa vigumu kwa waangalizi wa kimataifa kutegemewa
kushiriki kwa namna yoyote katika uchaguzi huo.
0 comments:
Post a Comment