January 08, 2016

Jumla ya Wananchi 1,572 wa Vijiji vya Michamvi Pingwe na Michamvi Kae wanatarajiwa kupata Maji safi na salama baada ya kukamilika kwa Mradi wa kuchuja Maji Chunvi kuwa Maji matamu.
Kukamilika kwa mradi huo kutawapunguzia Kero wananchi wa Vijiji vya Michamvi ambao kwa miaka mingi wamekumbwa na tatizo hilo bila ya msaada wowote.
Hayo yameelezwa na Waziri wa Uwezeshaji, ustawi wa Jamii,Vijana Wanawake na Watoto Zanzibar Zainab Omar Mohammed wakati akiweka Jiwe la Msingi la Mradi huo huko Michamvi wilaya ya Kusini Unguja.
Amesema uwekaji wa Jiwe la Msingi wa Mradi huo na kupata maji matamu ambayo yatawasaidia wananchi hao ni moja kati ya jitihada zinazofanywa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa lengo la kuwaondoshea shida ya upatikanaji wa maji wananchi wake.
“Malengo makubwa ya jitihada hizo ni kuwaondoshea kero Wananchi ya kukosekana kwa huduma hiyo ya maji safi ili waweze kushughulikia zaidi kazi za uzalishaji mali na maendeleo kwa lengo kuimarisha kipato chao” amesema Waziri Zainab.
Ameongeza kuwa eneo la Michamvi ni moja kati ya maeneo yanayokabiliwa na upatikanaji wa maji safi na salama na kwamba baada ya muda mfupi wananchi wataondokana na kero hiyo.
Akitoa taarifa juu ya Mradi huo Naibu Katibu mkuu Wizara ya Ardhi, Makaazi,Maji na Nishati Mustafa Jumbe amesema Mradi umetekelezwa na kugharamiwa kati ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Kampuni ya UST kutoka Ujerumani ambapo jumla ya Shilingi Millioni 475 za Kitanzania zinatarajiwa kutumika.
Amefafanua kuwa Kampuni ya UST imechangia Milioni 395 ambapo kwa upande wa Serikali ya Mapinduzi kwa kushirikiana na Wananchi wamechagia Millioni 80.
Jumbe amezitaja kazi zitakazofanyika kuwa ni pamoja na uchimbaji wa kisima,utiaji wa pampu,ujenzi wa kibanda cha kuwekea mitambo na ununuzi wa mitambo ya kusafishia maji chumvi kuwa matamu.
Akitoa nasaha Mkuu wa Wilaya ya Kusini Jabir Khamis Makame amewaomba wananchi wa Michamvi kuuenzi Mradi huo ili uweze kuwaletea matunda yaliyokusudiwa.
Uwekaji wa Jiwe la Msingi Mradi wa Kuchuja maji Chumvi kuwa Maji matamu ni moja ya matunda ya Mapinduzi ya Zanzibar ambayo lengo lake ni kuwakombo Wananchi na Umasikini ikiwemo kuwaletea maji safi na salama katika maeneo yao.



: Maelezo Zanzibar

0 comments:

Post a Comment