Kauli ya Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania
(TFF) Jamal Malinzi kutoitambua kamati inayosimamia shughuli za soka visiwani
Zanzibar, imewasha moto.
Itakumbukwa jana, akizungumza na waandishi wa
habari jijini Dar es Salaam, Malinzi alieleza msimamo wa TFF wa kuutambua
uongozi wa asili wa ZFA chini ya Rais aliyemaliza muda Ravia Idarous Faina,
badala ya kamati ya muda iliyoundwa kusimamia mpira wa miguu Zanzibar.
Aidha, Rais huyo alieleza kuwa TFF haiku
tayari kufanya kazi na kamati hiyo na kuongeza kuwa shirikisho hilo
halitahusika na lolote litakalotokea kwa ZFA chini ya kamati hiyo.
Kufuatia kauli hiyo, Makamu Rais wa ZFA
aliyemaliza muda wake Haji Ameir Haji, leo Januari 29 aliitisha mkutano na
waandishi wa habari katika hoteli ya Zanzibar Ocean View, na kumshutumu
Malinzi, huku akimtaja kuwa sehemu ya mgogoro wa ZFA.
Ameir, al maaruf ‘Bosi Mpakia’, alisema kwa
kauli yake, Malinzi ameonesha hadharani rangi zake halisi kwamba halitakii mema
soka la Zanzibar na yuko tayari kushirikiana na kikundi cha watu wachache ndani
ya ZFA kuhujumu soka la visiwa hivyo.
Ameir alimshangaa Malinzi kwa kuamua ‘kutia
ulimi puani’, ikizingatiwa kwamba yeye ndiye aliyeitisha kikao mwishoni mwa
mwaka jana kati ya uongozi wa kamati na viongozi wa juu wa ZFA jijini Dar es
Salaam kwa ajili ya kusafisha hali ya hewa iliyochafuka kisoka baada ya Ameir
kuwashtaki mahakamani viongozi wenzake wa juu wa chama hicho.
Ameir ndiye aliyewapandisha kizimbani, Rais wa
ZFA Ravia, Makamu wake anayefanyia kazi kisiwani Pemba Ali Mohammed na
Katibu Mkuu wa chama hicho Kassim Haji Salum, akiwatuhumu kwa matumizi
mabaya ya fedha za chama na kuvunja katiba.
Alifahamisha kuwa, TFF ilikutana na kamati
pamoja na akina Ravia, ikiwa mpatanishi kufuatia Shirikisho la Soka Afrika
kuiandikia ZFA na kuitahadharisha juu ya kesi zilizokuwa zimefunguliwa
mahakamani dhidi yake kwamba zinatishia kufutiwa uanachama wake shirikisho CAF.
Alisema baada ya kikao hicho, pande zote
zilikubaliana na kutoka na maazimio kadhaa, yanayozingatia ushirikiano kati yao
kwa lengo la kumaliza mgogoro uliopo ambao unachangia kulipeleka kaburini soka
la Zanzibar.
Aliyataja baadhi ya mambo waliyokubaliana,
kuwa ni pamoja na kuiachia kamati isimamie shughuli zote za soka ikiwemo
kuhakikisha ligi za madaraja yote zinachezwa, jambo ambalo tayari limefanyika.
Aidha, alisema Malinzi alipendekeza Ravia
(Rais) achague watu wengine watatu kuiongezea nguvu kamati katika kazi zake za
kuipitia na kuifanyia marekebisho katiba ya ZFA na hatimaye kuitisha uchaguzi
mkuu.
“Kama huu si unafiki ni kitu gani. Malinzi
alikuwa na maana gani kuiita kamati na ZFA Dar kama bado hana imani na upande
mmoja?” alihoji.
Ameir alisema yeye binafsi pamoja na kamati
hawana tatizo na TFF kumtambua Ravia kama Rais, kwani kimsingi ZFA yenyewe sasa
haipo kwani hakuna kamati tendaji ambayo kimsingi ndiyo inayoandaa mkutano mkuu
na uchaguzi.
“Uongozi wa ZFA umemaliza muda tangu mwishoni
mwa Disemba 2014, na hata muda walioongezewa Rais, makamu wake wawili na Katibu
Mkuu nao umemalizika, lakini hakuna kamati inayoweza kuitisha mkutano mkuu,
zaidi ya Mrajis wa Vyama vya Michezo kubariki kamati ya muda kusimamia soka kwa
sasa,” alifafanua.
“Mimi ninajitambua kuwa si kiongozi tena wa
ZFA lakini ninazungumza kama mtu mwenye kukitakia mema chama hicho tiofauti na
wenzangu ambao wametegema kuchuma fedha kupitia mgongo wa mpira wa miguu,”
alieleza kwa hasira.
Akizidi kuichambua kauli ya Malinzi, Ameir
alisema inaonesha wazi kwamba bosi huyo wa TFF amerubuniwa na viongozi
walioshtakiwa kwa lengo la kuona soka la Zanzibar linavurugika.
Ameir alikwenda mbali kwa kusema sasa
anakusudia kumburuza mahakamani Rais wa TFF baada ya kutoa kauli hiyo,
aliyoesema ni ya kupotosha, baada ya awali yeye binafsi kuwa msimamizi wa kikao
kilichozaa muafaka ulioipa Baraka kamati, ambayo jana ameikana.
Januari 29, 2016
0 comments:
Post a Comment