JESHI
la Polisi Mkoa wa Kusini Pemba, kwa pamoja na Chama cha Wananchi CUF, wamefikia
makubaliano ya pamoja, ya kutokuwepo kwa maandamano na mkutano wa hadhara wa
chama hicho, uliotarajiwa kufanyika Jumapili katika uwanja wa Tibirinzi.
Chama hicho kilitoa
taarifa ya maandamano ya kuunga mkono hutuba ya Katibu mkuu wa chama chao alipozungumza
na wa waandishi wa habari pamoja na
kulaani kitendo cha Mwenyekiti wa Tume ya uchaguzi Zanzibar, ZEC Jecha Salim
Jecha kuyafuta matokeo ya uchaguzi.
Kwa mujibu wa taarifa
zilizopatikana na mwandishi wa habari hizi, kikao cha kufikia mwafaka huo,
kilidumu kwa saa mbili, na kujitokeza hoja nzito baina ya maofisa wa Jeshi la
Polisi mkoa wa kusini Pemba na uongozi wa chama cha wananchi CUF.
Aidha taarifa hizo
zinaeleza kuwa, licha ya kufikia kwa makubaliano hayo, wanachama wa chama
hicho, wamepingana na uamuzi wa Jeshi la Polisi na viongozi wao, na kusema siku
ikifika wataingia barabarani kwa amani kufanya maandamano.
Hata hivyo wanachama hao
walisema, wanafanya hivyo, kutokana na wenzao wa chama cha Mapinduzi CCM
Unguja, juzi Januari 11, waliruhusiwa kufanya maandamano ya amani, kama
wanayotaka kuyafanya wao.
Katibu wa CUF wilaya ya
Chakechake, Saleh Nassor Juma, alikiri kwamba baada ya kikao kizito,
wamekubaliana na Jeshi la Polisi kusitisha maandamano na mkutano wa hadhara wa
chama chao.
“Ni kweli tumekubaliana
na Jeshi la Polisi kwamba, maandamano na mkutano yasiwepo, lakini ni kweli
wanachama wetu wapinga hilo na wao wanasubiri siku ifike wafanye maandamano ya
amani’’,alisema.
Katibu huyo alisema, kazi
wanayoendelea kuifanya ni kuwahamasisha waatii amri ya Jeshi la Polisi, pamoja
na viongozi wao wa CUF, ingawa alisema kama wakiendelea kukataa wataungana nao.
“Unajua sisi kama
viongozi wa CUF, tumetii amri ya Jeshi la Polisi tusifanye maandamano na
mkutano wa hadhara, na wananchama wetu tunawasisitiza sana wasishiriki, lakini
kama wakiwa kicha ngumu, inabidi na sisi tuwe mbele’’,alisistiza.
Hata hivyo Katibu huyo wa
CUF wilaya ya Chakechake, alisema kiliochobakia ni kuwasiliana na uongozi wa
ngazi ya juu wa CUF Unguja, ili na wao watoe baraka ya kutoshiriki maandamano
na mkutano huo.
Mapema Mkurugenzi mipango
na uchaguzi wa chama cha CUF Omar Ali Shehe, alisema hana taarifa za kwamba
Jeshi la Polisi limepiga marufuku maandamano yao ya amani, kwa vile alikuwa
hajapokea taarifa hizo.
Kamanda wa Polisi mkoa wa
kusini Pemba, Shehan Mohamed Shehan alisema yeye anachofahamu ni makubaliano
baina yao na uongozi wa chama cha CUF ya kusitisha maandamano na mkutano huo.
Alisema, Jeshi la Polisi
halina taarifa ya wanachama wa CUF kwamba wataingia barabarani kupinga amri ya
viongozi wao na ya Jeshi la Polisi, na hasa baada ya kikao kizito.
“Sisi kama Jeshi la
Polisi tumeshakubaliana na CUF kwamba kusiwe na maandamano wala mkutano wa
hadhara wa kuunga mkono hutuba ya kiongozi wao, na tunatarajia na wanachama
watii agizo hilo’’,alifafanua.
Juzi chama cha wananchi
CUF kilitoa taarifa kwa waandishi wa habari kwamba, Jumapili ijayo ya Januari
17, kinatarajia kufanya maandamano ya amani yanayotarajiwa kuanzia njia ya
Uwanja wa ndege na kumalizia kwa mkutano wa hadhara, viwanja vya Tibirinzi
Chakechake Pemba kuunga mkono hutuba ya Katibu Mkuu wao.
: Haji Nassor, Pemba
0 comments:
Post a Comment