Serikali imesema uamuzi wa kurudia
uchaguzi wa urais Zanzibar ni halali na wa kisheria na kwamba wanaotafuta
suluhu nje ya Katiba, wanakosea.
Kauli hiyo ilitolewa mjini hapa jana na
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira, January Makamba alipokuwa
akihitimisha majadiliano ya kuchangia hotuba ya Rais John Magufuli.
Alisema uchaguzi ulifutwa kisheria na Tume ya
Uchaguzi Zanzibar (ZEC) kwa Tangazo la Serikali Namba 6587. Makamba alisema
Katiba ya Zanzibar, imeeleza wazi kuwa hakuna mamlaka ambayo itahoji uamuzi wa
tume, hata kama ni Mahakama. Alisema akidi ilitimia wakati tume inafikia hatua
hiyo.
Waziri huyo alisema wanaotaka kutumia
suala hilo kuleta vurugu Zanzibar, damu za Watanzania zitawalilia. Alisema
viongozi wakuu wa nchi, wamefanya kazi kubwa katika kulitafutia ufumbuzi suala
hilo na hivyo ieleweke kuwa ZEC na NEC ni tume zinazojitegemea.
Alisisitiza NEC haiwezi kuingilia uamuzi wa
ZEC, kwani uchaguzi wa rais uliofanyika kwa siku moja Tanzania Bara na
Zanzibar, umekuwa ukiendeshwa na Tume mbili tofauti. Alisema uchaguzi huo,
ulifanywa na tume tofauti na hata wino uliotumika katika chaguzi hizo ni
tofauti .
Alisema wajibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ni
kuhakikisha kuwa amani na utulivu, vinalindwa Zanzibar katika marudio ya
uchaguzi unaotarajiwa kufanyika Machi 20 mwaka huu.
Oktoba 28 mwaka jana, Mwenyekiti wa ZEC, Jecha
Salim Jecha, alitoa “Taarifa Kwa Umma ya Kufuta Uchaguzi wa Zanzibar”.
Katika taarifa hiyo, Jecha Salim Jecha alisema “Mimi
nikiwa Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar, nimeridhika kwamba uchaguzi
huu haukuwa wa haki na kuna ukiukwaji mkubwa wa sheria na taratibu za uchaguzi.
Hivyo, kwa uwezo nilionao natangaza rasmi kwamba uchaguzi huu na matokeo yake
yote yamefutwa na kwamba kuna haja ya kurudia uchaguzi huu”
0 comments:
Post a Comment