January 11, 2016

Makamo  Mwenyekiti wa CCM  Zanzibar, Dkt. Ali Mohamed Shein amesema suala la kurudiwa kwa uchaguzi wa Zanzibar halina njia ya mkato hivyo wananchi wasubiri Tume ya uchaguzi Zanzibar ZEC kutangaza siku ya uchaguzi huo.
Amesema uchaguzi mkuu uliopita umefutwa kisheria na kwa kuzingatia matakwa ya Kikatiba hivyo utarudiwa kwa kufuata muongozo wa chombo kilichopewa mamlaka hiyo ambacho ni ZEC.
Msimamo huo ameutoa leo katika kilele cha matembezi ya UVCCM Zanzibar huko katika Viwanja vya Maisara amesema kuwa yeye bado ni Rais halali wa Zanzibar kwa mujibu wa Katiba ya Mwaka 1984 hivyo hakuna haja ya baadhi ya wanasiasa kuendelea kutoa vitisho na hujuma za kisiasa zinazolenga kuhatarisha amani ya nchi.
Dkt. Shein amewataka wananchi wasikubali kuhadaiwa na baadhi ya wanasiasa wanaojali maslahi binafsi badala ya maendeleo na mipango endelevu ya kuwaondoa wananchi katika hali ya umasikini.
Amesema kuwa kiongozi yeyote anayetaka kuwa Rais wa Zanzibar lazima afuate utaratibu halali wa kidemokrasia bila ya kutumia njia za mkato na udanganyifu usiofaa katika siasa za zama hizi.
Aidha amesema kuwa vijana hao wanajukumu la kuendelea  kuwahamasisha vijana wengine  kulinda na kuthamini Mapinduzi ya Zanzibar ya Januari ya mwaka 1964.
Mwenyekiti wa UVCCM Taifa, Sadifa  Juma Khamis amesema kuwa umoja huo utaendelea kuenzi na kulinda Mapinduzi ya Zanzibar bila ya woga wowote kwani waasisi wa dhana hiyo walitoa sadaka maisha yao kwa ajili ya kuweka uhuru wa kudumu kwa wananchi wa Zanzibar.
Amesema katika kipindi cha miaka 52 ya Mapinduzi ya Zanzibar nchi imepata mafanikio makubwa yaliyofanywa na serikali inayoongozwa na wananchi wazalendo wa visiwa vya Zanzibar baada ya kujitawala wenyewe kutoka katika mikono ya walowezi.
Naye Kaimu Katibu Mkuu wa UVCCM  Taifa, Shaka Hamdu Shaka amesema Matembezi ya kuenzi miaka 52 ya mapinduzi ya Zanzibar  yameamsha ari na nguvu kwa vijana wa umoja huo kuendelea kujenga msimamo dhabiti wa kushiriki harakati za kulinda mapinduzi bila ya woga.
Amesema bado UVCCM ina imani na serikali ya Zanzibar ya awamu ya saba chini ya uongozi wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Ali Mohamed Shein katika kusimamia vyema dhana ya mapinduzi kwa kulinda amani na utulivu wan chini.
Shaka ameeleza kwamba matembezi hayo ya siku tatu yaliyoanzia katika Kijiji cha Kitope Mkoa wa Kaskazini Unguja yakiwa na vijana zaidi ya 2000 kutoka mikoa mbali mbali ya Zanzibar na baadhi ya mikoa ya Tanzania bara.
Kaimu Katibu Mkuu huyo amesema umoja huo unaendelea kuunga mkono msimamo wa CCM wa kushiriki katika uchaguzi wa Marudio wa Zanzibar wakiamini kuwa fursa hiyo ndio njia pekee ya kutafuta ufumbuzi wa kudumu wa kumaliza mkwamo wa kisiasa uliopo Zanzibar.





0 comments:

Post a Comment