YA KUUKARIBISHA
MWAKA MPYA WA 2016.
NduguWananchi,
Assalam
Aleikum,
Kwa hakika tuna wajibu
wa kumshukuru Mwenyezi Mungu, Mtukufu, Muweza wa Kila Kitu kwa kutupa uhai
tukaweza kufika hadi siku hii ya leo tunapouaga mwaka 2015 na
kuukaribisha mwaka mpya wa 2016. Hii ni neema kubwa aliyoturuzuku
Mola wetu, Subhana Wataala kwani katika kipindi kama hiki mwaka jana, tulikuwa
na wenzetu ambao kwa hivi sasa wamekwishatangulia mbele ya haki. Tumuombe
Mwenyezi Mungu awasamehe makosa yao na awape malazi mema. Na sisi tulio
hai atujaalie khatma njema.
Wakati mwaka 2015
unamalizika ni vyema japo kwa muhtasari tukatafakari baadhi ya masuala muhimu
tuliyokabiliana nayo katika mwaka huo. Hatua hiyo, itatuwezesha kufanya
tathmini ya mafanikio na changamoto tulizokumbana nazo ili tuweze kujipanga na
kuweka dhamira ya kuzifanyia kazi kwa lengo la kupiga hatua zaidi za maendeleo
kwa mwaka ujao.
Ndugu
Wananchi,
Katika mwaka wa 2015,
nchi yetu ilikuwa na hali ya amani na utulivu jambo ambalo tunapaswa kumshukuru
Mwenyezi Mungu kwa kutupa neema hiyo ambayo imetuwezesha kutekeleza kwa mafanikio
mipango yetu ya maendeleo ikiwemo Dira ya Maendeleo ya Mwaka 2020, MKUZA
II, Malengo ya Milenia na Ilani ya Uchaguzi Mkuu ya CCM ya mwaka 2010 –
2015 ambayo tuliweza kuitekeleza kwa asililmia 90. Kuwepo kwa amani
kumetuwezesha wananchi kuendelea na shughuli zetu za kila siku kwa
utulivu. Kutokana na amani na utulivu uliopo wageni wengi
wameendelea kuitembelea nchi yetu. Jumla ya watalii 254,699
waliitembelea Zanzibar katika kipindi cha Januari-Novemba, 2015 na kupelekea sekta
hii kuimarika kwa kiasi kikubwa.
Kufuatana na takwimu
za robo mbili za mwanzo wa mwaka 2015, uchumi wetu umeendelea kuimarika.
Sura halisi itafahamika baada ya kumalizika kabisa kwa mwaka huu na tathmini
kamili ya hali ya uchumi kufanywa. Kwa upande mwengine, huduma za jamii
zikiwemo upatikanaji wa maji safi na salama, huduma za afya pamoja na elimu
zimeimarika.
Ndugu
Wananchi,
Katika mwaka huu,
tumepiga hatua kubwa katika kuimarisha miundombinu. Tumeweza kumaliza ujenzi wa
barabara muhimu na kuzizindua Unguja na Pemba, ikiwemo barabara ya Wete Gando
na Wete Konde. Tumeimarisha bandari zetu pamoja na viwanja vya ndege. Sote ni
mashahidi wa kazi kubwa tuliyoifanya katika kukiimarisha Kiwanja cha Ndege cha
Kimataifa cha Abeid Amani Karume pamoja na Kiwanja cha ndege cha Pemba ambacho
tayari tumekitia taa za kurukia ndege. Katika mwaka 2015, tulikamilisha na
kuzindua mradi wa ujenzi wa maegesho ya ndege (Apron) na njia za kupitia ndege
(taxiway) katika Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Abeid Amani Karume.
Kadhalika, tumeendeleza ujenzi wa jingo la abiria litalokuwa na uwezo wa
kuchukua abiria milioni 1.6 kwa mwaka.
Hatua tuliyofikia
katika ujenzi wa viwanja hivi tayari imepelekea kuwepo kwa ongezeko kubwa la
idadi ya ndege za Kimataifa zinazokuja Zanzibar, jambo ambalo limepelekea
kuimarika kwa sekta ya utalii na shughuli za biashara.
Ndugu
Wananchi,
Miongoni mwa masuala
muhimu ya maendeleo ambayo nchi yetu imeyapata katika mwaka uliomalizika ni
kufanikiwa kwa lengo la Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Awamu ya Saba, la
kuwapatia meli mpya wananchi wa Zanzibar. Serikali iliweka dhamira ya
dhati ya kupambana na tatizo la uhaba wa vyombo vya kuaminika vinavyofanya
safari zake kati ya Unguja, Pemba na Dar es Salaam. Tulifanikiwa
kuitengenezesha meli mpya, yenye mitambo ya kisasa katika Kampuni ya “Daewoo
International” ya Jamhuri ya Korea ambayo ina utaalamu na uzoefu mkubwa wa
kutengeneza meli.
Tayari meli hiyo
tuliyoipa jina la MV Mapinduzi II, iliwasili nchini tarehe 2 Disemba,
2015. Nasaha zangu kwenu nyote wananchi ni kuwa, tuithamini na kuienzi
meli yetu hiyo. Tukumbuke msemo wa Marehemu Mzee Abeid Amani Karume, kuwa “kithamini
kilicho chako mpaka usahau cha mwenzako” .
Katika mwaka 2015,
tumefanya juhudi kubwa katika kuhakikisha kuwa dhamira yetu ya kujenga bandari
ya Mpiga Duri tunaanza kuitekeleza. Juhudi kubwa zimefanywa katika
kutafuta fedha za mradi huu. Hivi sasa Serikali inakamilisha mazungumzo
ya kupata fedha kwa njia ya mkopo kutoka “Exim Bank” China. Kwa kuanzia
ujenzi wa bandari hii, utachukua eneo la mita 300 kutoka Kusini kwenda
Kaskazini na utajumuisha ufukiaji wa bahari, eneo lenye urefu upatao mita
490. Ujenzi wa bandari hii utategemea kuanza wakati wowote katika mwaka
2016. Ujenzi huo utakapomalizika utapunguza msongamano uliopo katika
bandari ya Malindi na utaimarisha kwa kiasi kikubwa ukuaji wa biashara hapa
Zanzibar. Kadhalika, gati hiyo itatoa ajira kwa wananchi na kutoa mchango
mkubwa katika ukuaji wa uchumi wetu.
Vile vile,
katika mwaka huu unaomalizika tumepata mafanikio katika juhudi zetu za
kusambaza huduma za umeme vijijini. Vijiji mbali mbali kama vile Kijini
na Mbuyu Tende katika Mkoa wa Kaskazini Unguja vimepatiwa huduma hizo. Aidha,
kwa kuwatumia wataalamu wazalendo tumeweza kuufikisha umeme huko Kisiwa Panza
na Kisiwa cha Makoongwe kwa upande wa Pemba.
Kadhalika,
katika mwaka 2015, tumetekeleza kwa mafanikio miradi ya maji safi na salama
katika maeneo mbali mbali, Unguja na Pemba. Tumeshuhudia ongezeko la
uchimbaji wa visima katika maeneo kadhaa. Vile vile, tunatarajia kulipatia
ufumbuzi, tatizo la maji safi na salama katika Manispaa ya mji wa Zanzibar
kufuatia kutiwa saini Mkataba wa Mradi wa Maji Mjini tarehe 29 Disemba, 2015.
Mradi huo utagharimu
jumla ya Dola za Marekani 21,000 zikiwa ni mkopo kutoka Benki ya
Maendeleo ya Afrika (AfDB) na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itachangia
asilimia 10. Kampuni zinazohusika ni NSPT LTD na SPENCON SERVICES LTD
zilizosajiliwa nchini Tanzania. Maeneo yatakayofaidika ni Mji Mkongwe na
maeneo yanayopakana na mji huo.
Tumeanza kuifanyia
kazi changamoto ya ukosefu wa huduma za umeme katika sehemu tulizochimba
visima, jambo ambalo kwa kiasi kikubwa huathiri juhudi zetu za
kuwafikishia wananchi huduma hizi muhimu. Matumaini yangu ni kuwa ifikapo
mwishoni mwa mwaka 2016 changamoto hii itakuwa imeshapatiwa ufumbuzi na
kukidhi matarajio ya wananchi.
Ndugu
Wananchi,
Kwa upande wa huduma
za afya, katika mwaka 2015 tumeziimarisha huduma hizo kwa kuongeza kasi
ya kusomesha wataalamu, upatikanaji dawa na huduma mbali mbali pamoja na
kuziimarisha hospitali zetu kwa kutekeleza miradi mbali mbali ya ujenzi.
Katika mwaka wa 2015, tulianza kuijenga upya hosptali ya Abdalla
Mzee Pemba kwa msaada wa Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China. Ujenzi huo
utakamilika mwaka 2016. Hivi sasa tunaendelea na uimarishaji wa Hosptali
ya Mnazi Mmoja kwa kujenga majengo mapya na kuongeza kasi ya utoaji wa huduma
mpya ili tufikie azma yetu ya kuifanya hosptiali hii kuwa ya rufaa.
Katika kipindi hiki tumeziondoa gharama za kuchangia huduma za
uchunguzi wa maradhi kwa kutumia “X-Ray”, “CT-Scan” na “Ultra Sound” na sasa
zinatolewa bila ya malipo kwa wananchi wote. Katika mwaka ujao wa 2016
juhudi zitafanywa za kuondoa kuchangia huduma za uchunguzi wa maabara, ili nazo
ziwe bila ya malipo.
Katika mwaka 2015
tumepata mafanikio makubwa kwa upande wa elimu. Tumemaliza na kuanza upya
miradi ya ujenzi wa skuli mbali mbali na kuongeza fani za mafunzo katika vyuo
vikuu na taasisi za elimu ya juu. Vile vile, tumeanza kutekeleza lengo
letu la kuondoa utaratibu kwa wazazi kuchangia gharama za elimu maskulini
kama nilivyotangaza tarehe 12 Januari, 2015. Lengo letu ni kuifanya elimu
ya msingi kuwa bure huku tukiandaa utaratibu ili elimu ya sekondari nayo iwe
bure kama ilivyodhamiriwa na Muasisi wa Mapinduzi yetu ya 1964.
Katika mwaka 2015,
tulifikia uamuzi ya kuwapatia pensheni ya kila mwezi wazee wetu wote waliofikia
umri wa miaka 70 bila ya kujali kama waliwahi kuajiriwa Serikalini au
hawakuajiriwa. Hatua hiyo itaanza kutekelezwa kuanzia mwezi April mwaka
2016. Ni wajibu wetu kuwatunza wazee wetu ambao wamefanya kazi kubwa ya
kuijenga nchi yetu katika ujana wao.
Ndugu
Wananchi,
Katika mwaka 2015
tulipanga na kuanza kutekeleza kwa kasi, mipango ya ujenzi wa miji na majengo
ya kisasa katika sehemu mbali mbali ili kuweza kujenga taswira mpya ya
Zanzibar katika kipindi kifupi kijacho.
Serikali kupitia ZIPA
ilipanga kutekeleza miradi mitano ambayo baadhi yake tayari imeshapata
wawekezaji na kuanza kutekelezwa katika eneo la Fumba. Miradi hiyo
inahusisha ujenzi wa miji ya kisasa ya makaazi, uwekezaji wa viwanda vidogo
vidogo, ujenzi wa kituo cha kimataifa cha mikutano na maonyesho ya biashara.
Serikali, kwa kushirikiana na Kampuni za “Union Property Developer” na “Coastal
Dredging” inaendelea na ujenzi wa barabara katika maeneo yaliyopangwa
kuendelezwa kwa kujengwa mji mpya wa kisasa huko Fumba. Kwa sasa barabara
kuu zenye urefu wa kilomita 13 zimo katika hatua mbali mbali za ujenzi.
Jumla ya nyumba 1,300 zinatarajiwa kujengwa kwa ajili ya kuuzwa kwa
wazalendo katika kipindi cha mwaka mmoja ambapo kwa kuanzia, nyumba 150
zitaanza kujengwa mwezi wa Februari, 2016.
Kwa upande wa Mkoa wa
Kaskazini Unguja, Mradi wa ujenzi wa mji wa kisasa wa kibiashara pamoja na
hoteli kubwa ya nyota tano, utakaojengwa huko
Ma temwe umeanza kutekelezwa na
unatarajia kuwekeza jumla ya Dola za Marekani milioni 800. Kampuni ya “Pennyroyal
ya Gibralter” ndiyo inayotekeleza mradi huo.
Kwa upande mwengine
katika mwezi wa Novemba 2015, Serikali ilitiliana saini Mkataba na Kampuni ya
“Quality Group Limited” ambayo itaanzisha mradi mkubwa wa kuendeleza Hoteli ya
Bwawani na maeneo yanayoizunguuka. Mradi huo utawekeza mtaji wa Dola za
Marekani kiasi cha Milioni 200 na utahusisha kulifanyia ukarabati mkubwa jengo
la Hoteli ya Bwawani na kuliwezesha kutoa huduma za hoteli ya nyota tano. Jengo
hili la hoteli litaimarishwa ili kuhifadhi kielelezo cha mafanikio cha
Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ya 1964.
Kadhalika, Serikali
imeidhinisha mradi wa upanuzi wa Hoteli ya Mtoni Marine, unaohusisha
utengenezaji wa ufukwe kwa ajili ya mapumziko ya wageni na wenyeji.
Upanuzi huo, vile vile, unahusisha uanzishwaji wa mji mdogo wa kisiwa kwa ajili
ya watu wenye uwezo wa kifedha na hivyo kupelekea Serikali kukusanya mapato
yatayotokana na umiliki wa majengo katika mji huo. Mwaka 2015, ulibeba shughuli
nyingi za uanzishwaji wa ujenzi wa miji mipya.
Sambamba na juhudi
hizo zinazochukuliwa na ZIPA za kushajihisha wawekezaji katika ujenzi wa miji
ya kisasa, Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar (ZSSF) nao unaendelea na juhudi
za kubadillisha taswira ya Zanzibar kwa kuwekeza katika ujenzi wa majengo ya
kisasa katika eneo la Mbweni. Mradi huu umejumuisha ujenzi wa jumla
ya majengo 18 ya ghorofa 7 kila moja, yatakayokuwa na nyumba 252. Ujenzi
wa majengo hayo umeshaanza. Wakati tunamaliza mwaka huu 2015, tunapaswa
kujipongeza kwa kufanikisha ujenzi wa Viwanja vya Watoto, Kiwanja cha Kariakoo
kwa Unguja na Tibirinzi kwa upande wa Pemba. Kukamilika kwa ujenzi wa Mnara wa
Kumbukumbu ya Miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar katika eneo la Michenzani,
kumeiletea haiba mpya mji wetu wa Zanzibar na umekuwa ni kielelezo kizuri cha
kumbukumbu ya Mapinduzi yetu ya 1964.
Ndugu
Wananchi,
Ili mafanikio haya
tuliyoyapata yawe endelevu, napenda nikumbushe kuhusu umuhimu wa kuitunza
miundombinu yetu yote ya maendeleo ambapo fedha nyingi zinatumika katika
kuitengeneza kwa ajili ya maendeleo yetu. Inasikitisha kuona kwamba
katika mwaka uliomalizika, baadhi ya watu waliendeleza vitendo vya kuharibu
miundombinu katika maeneo mbali mbali kwa kuweka mbele maslahi yao binafsi na
kusahau wajibu wa kutanguliza maslahi yetu sote.
Katika baadhi ya
maeneo ya nchi yetu, watu hao walikata nyaya za umeme na kusababisha hasara kwa
shirika la umeme (ZECO) na usumbufu kwa wananchi kwa kukosa huduma hiyo.
Aidha, katika maeneo mengine vitendo vyao vimesababisha kukosekana kwa
huduma za maji safi na salama. Natao wito kwa wananchi wote ili tuwe
walinzi wa miundombinu yetu na tusichelee kuwafichua wale wote wanayoiharibu.
Ndugu
Wananchi,
Tunamshukuru Mwenyezi
Mungu kwa kutupa neema ya mvua ambayo imetuwezesha kupata mazao ya
chakula na biashara hasa zao la karafuu katika mwaka uliomalizika. Kwa
mara nyengine tena napenda niwashukuru wakulima wetu kwa jitihada zao katika
kilimo, hali ambayo imesaidia sana kuwapo kwa uhakika wa mazao ya chakula
zikiwemo ndizi, muhogo, viazi, matunda na aina za mboga. Kadhalika, natoa
shukurani kwa wakulima wa mpunga wa kutegemea mvua kwa jitihada zao, ingawa kwa
bahati mbaya hali ya mavuno kwa mwaka uliomalizika haikuwa nzuri sana.
Tayari maandalizi ya
kilimo cha mpunga wa kutegemea mvua kwa mwaka huu yamekwishaanza katika mabonde
mbali mbali ya Unguja na Pemba kwa hatua ya kuchimbua mashamba.
Serikali inaendelea kutoa ruzuku kwa huduma za matrekta na pembejeo za kilimo
kwa wakulima ambapo kwa msimu wa mwaka 2015/2016, tani 750 za mbolea na
lita 15,000 za dawa ya kuulia magugu zimekwishanunuliwa.
Natoa wito kwa
wakulima wetu kuzitumia fursa zilizowekwa na Serikali ili kuongeza tija katika
kilimo chetu. Kadhalika, nawasihi wafuate maelekezo ya maafisa ugani ya
kuzingatia misingi ya kilimo bora kwa kutayarisha mashamba kwa wakati, kutumia
mbegu bora, mbolea na dawa za kuulia wadudu ili tupate mazao mengi
yatakayotuwezesha tupunguze uagiziaji wa mchele hatua kwa hatua kutoka nje ya
nchi.
Ndugu
wananchi,
Kuhusu zao la karafuu,
napenda nitoe pongezi kwa wakulima wa karafuu kwa jitihada zao na kushirikiana
na Serikali katika kuliendeleza zao hilo. Wakulima wetu wameitikia
vyema wito wa Serikali wa kuuza karafuu zao katika vituo vya ZSTC ambapo katika
msimu wa ununuzi wa karafuu 2015/2016, hadi kufikia mwezi Novemba, 2015 jumla
ya tani 962.7 za karafuu zenye thamani ya TShs. Bilioni 13.471 zimenunuliwa
katika vituo vya ununuzi wa karafuu vya ZSTC Unguja na Pemba. Kwa mara
nyengine nalipongeza Shirika la Biashara la Taifa (ZSTC) kwa kazi nzuri
waliyoifanya ya kuliendeleza zao la karafuu pamoja na vikosi vyetu vya ulinzi
na wananchi wote kwa kupambana na magendo ya karafuu. Kwa lengo la kuzidi
kuliimarisha zao la karafuu na kuendeleza zaidi zao hili. Mnamo mwezi wa
August, 2015 tulizindua Mfuko wa Maendeleo ya Karafuu Zanzibar kwa lengo
la kuliendeleza zaidi zao hili. Kupitia mfuko huu, tuna matumaini
ya kuongeza ufanisi katika kulishughulikia zao la karafuu ili kuongeza tija.
Ndugu
Wananchi,
Mwaka 2015 ulikuwa ni
mwaka wa Uchaguzi Mkuu ambapo tarehe 25 Oktoba, wananchi wa Zanzibar
walishiriki katika kuwachagua Viongozi kwa upande wa Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Uchaguzi Mkuu
ulitanguliwa na kampeni za vyama vilivyoshiriki uchaguzi huo na wananchi
walishiriki kwa wingi katika kampeni zake.
Uchaguzi wa Viongozi
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania uliosimamiwa na Tume ya Uchaguzi ya Taifa ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania umemalizika na Chama cha Mapinduzi kimepata
ushindi mkubwa. Nampongeza Mheshimiwa Dk. John Pombe Magufuli kwa
kuchaguliwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mheshimiwa Samia
Suluhu Hassan kwa kuchaguliwa kuwa Makamu wa Rais. Kwa upande wa Zanzibar
Tume ya Uchaguzi uliufuta uchaguzi huu hapo tarehe 28 Oktoba, 2015, baada ya
kubainika kutokea kwa kasoro kadhaa kama zilivyoelezwa na Tume hiyo.
Aidha, uamuzi huo wa Tume ulitangazwa katika Gazeti Rasmi la Serikali la tarehe
6 Novemba, 2015 kwamba Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar imeyafuta matokeo yote ya
Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar wa tarehe 25 Oktoba, 2015 na kwamba uamuzi wa Tume wa
tarehe nyengine ya kurudiwa Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar utatangazwa baadae.
Aidha, katika suala
zima la hali ya kisiasa ya Zanzibar, iliyojitokeza baada ya kufutwa kwa
Uchaguzi Mkuu, viongozi wenu tulishauriana tukutane ili tufanye mazungumzo ya
kutafuta suluhu kwa njia ya amani, ili nchi yetu iendelee kuwa na amani, umoja
na mshikamano. Hatimaye tulikubaliana tuanze mazungumzo hayo.
Mazungumzo haya yanatuhusisha viongozi
sita. Viongozi hao ni mimi nikiwa Mwenyekiti, Makamu wa Kwanza wa Rais,
Mheshimiwa Maalim Seif Sharif Hamad na Mheshimiwa Balozi Seif Ali Iddi, Makamu
wa Pili wa Rais wakiwa wajumbe. Wajumbe wengine ni Rais Mstaafu wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Ali Hassan Mwinyi, Rais Mstaafu wa
Zanzibar wa Awamu ya Tano Dk. Salmin Amour Juma na Rais Mstaafu wa Zanzibar wa
Awamu ya Sita Dk. Amani Abeid Karume. Mazungumzo hayo yamefikia hatua
kubwa na bado yanaendelea. Taarifa kamili ya mazungumzo hayo itatolewa mara tu
yatakapokamilika.
Ndugu
Wananchi,
Kama inavyofahamika
kuwa kila mwaka inapofika mwezi wa Januari, huwa tuna maadhimisho ya
sherehe za Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ya Januari, 12 mwaka 1964.
Katika mwezi wa Januari wa mwaka 2015, tuliadhimisha sherehe za miaka 51 ya
Mapinduzi kwa matukio mbali mbali yaliyojumuisha uzinduzi na uwekaji wa mawe ya
msingi wa miradi ya maendeleo kwa Unguja na Pemba. Wengi wetu,
tulishiriki katika maadhimisho ya siku ya kilele, tarehe 12 Januari, 2015
kwenye Uwanja wa Amaan na sherehe hizo zilifana sana.
Tarehe 12 Januari,
2016, panapo majaaliwa tutaadhimisha miaka 52 ya Mapinduzi, ambapo kama
kawaida, sherehe hizo zitatanguliwa na matukio mbali mbali ya shughuli za
uzinduzi wa miradi ya maendeleo na uwekaji wa mawe ya msingi. Wito wangu
kwa wananchi wote ni kujitokeza kwa wingi katika matukio mbali mbali
yaliyopangwa katika maadhimisho hayo. Tukumbuke kuwa Mapinduzi yetu ni
kielelezo muhimu cha ukombozi wa nchi yetu na uzalendo. Aidha, kushiriki
kwetu kwenye sherehe ya maadhimisho haya ni hatua ya kuyaendeleza malengo ya
Mapinduzi kwa shabaha ile ile waliokuwa nayo waasisi wetu.
Ndugu
Wananchi,
Wakati tunapoukaribisha
mwaka mpya na tukiwa katika maandalizi ya sherehe za miaka 52 ya Mapinduzi,
napenda nisisitize umuhimu wa kuendeleza usafi wa mazingira katika maeneo
tunayoishi. Mazingira yaliyo machafu ni chanzo kikubwa cha maradhi mbali mbali
ya miripuko ikiwa ni pamoja na maradhi ya kipindupindu. Taarifa kutoka Wizara
ya Afya zinaeleza kuendelea kuwepo kwa maradhi ya kipindupindu katika baadhi ya
maeneo nchini na hali bado si ya kuridhisha sana. Hata hivyo, Serikali
inachukua hatua za kukabiliana na maradhi hayo kwa kuendeleza kambi za matibabu
na kutoa elimu ya afya juu ya namna ya kujikinga nayo.
Natoa wito kwa
wananchi nyote mzingatie kanuni za afya ikiwa ni pamoja na kuimarisha usafi,
kutotupa taka ovyo, kuepuka kuweka bidhaa chini hasa katika kipindi cha
mvua na kuhifadhi vyakula hasa vinavyouzwa barabarani. Aidha, Baraza la
Manispaa, Mabaraza ya miji kwa Pemba na Halmashauri zote za wilaya zichukue
hatua ya kusimamia uzoaji wa taka na kuzipeleka katika maeneo yaliyotengwa
pamoja na kuishughulikia misingi ya maji machafu kama hatua ya dharura ya
kukabiliana na maradhi ya mripuko. Sote tushiriki katika kuisafisha
Miji yetu na maeneo tunayoishi hapo tarehe 3 Januari, 2016, kama ilivyopangwa
katika ratiba ya Maadhimisho ya Sherehe za Mapinduzi kwa mwaka huu.
Ndugu
Wananchi,
Namaliza risala yangu,
kwa kukukumbusheni kwamba kesho tarehe 1 Januari ni siku yetu ya kujitokeza
sote kufanya mazoezi. Tujitokezeni kwa wingi. Nakutakieni kheri ya
mwaka mpya viongozi wote, wananchi, nchi marafiki, washirika wetu wa maendeleo
pamoja na mashirika ya Kimataifa kupitia mabalozi na wawakilishi waliopo
nchini. Namuomba Mwenyezi Mungu atujaalie kheri, baraka na neema nyingi katika
mwaka mpya wa 2016. Atuzidishie amani, umoja na masikilizano. Atujaalie
uwezo zaidi wa kuitekeleza mipango yetu kwa ufanisi ili kuimarisha uchumi na
ustawi wa maendeleo ya nchi yetu.
Ahsanteni kwa kunisikiliza.
0 comments:
Post a Comment