Kampuni ya Uwekezaji katika Sekta ya Mafuta na
Gesi kutoka Jamuhuri ya Watu wa China iko tayari kushirikiana na Serikali
ya Mapinduzi ya Zanzibar kuendeleza
miradi ya pamoja kwenye sekta hizo iwapo itapatiwa fursa katika mpango wa
uendelezaji wa miradi ya pamoja.
Mkuu wa Taaluma ya Miamba kutoka Kampuni
hiyo ya Kimataifa ya CNOOC Cui
Hanyun akiuongoza Ujumbe wa Viongozi Watano wa Kampunin hiyo pamoja na Balozi
Mdogo wa China aliyepo Zanzibar Xie Yun
Liang amesema hayo wakati wa mazungumzo yao na Makamu wa Pili wa Rais wa
Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Ofisini Vuga Mjini Zanzibar.
Hanyun amesema Kampuni hiyo yenye kutoa huduma
katika Mataifa tofauti Ulimwenguni pia inajihusisha na uwekezaji katika Benki
za Ufukweni { Off Show Banking }.
Amesema Uongozi wa Kampuni hiyo umeridhika na
mazingira bora ya Visiwa vya Zanzibar na kushawishika kutaka kuwekeza
miradi yao ili kuunga mkono hatua za SMZ za kuwashawishi wawekezaji wa
ndani na nje ya Nchi kuanzisha miradi yao ya kiuchumi katika sekta tofauti
Nchini.
Mtaalamu huyo wa Miamba wa CNOOC amemueleza
Balozi Seif kwamba Kampuni hiyo iko tayari kuweka nguvu zaidi katika
sekta ambayo Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaonyesha msisitizo kwa mujibu
wa mahitaji halisi ya Taifa na Wananchi walio wengi.
Hanyun amefahamisha kwamba Serikali ya
Jamuhuri ya Watu wa China imeshatoa baraka na kuyaruhusu Makampuni ya Nchi hiyo
kuanzisha miradi ya Benki za Ufukweni kwa vile tayari imeshakuwa na
wataalamu na uzoefu wa kutosha wa miaka mingi kwenye sekta hizo.
Naye Meneja wa Biashara wa Kampuni hiyo Ukanda
wa Bara la Amerika Hu Gencheng alieleza kwamba Kampuni hiyo mbali ya uzalishaji
pia imekuwa ikipokea Gesi kutoka Mataifa ya Indonesia, Qatar, na
Autralia.
Kwa upande wa Bara la Afrika Gencheng
alisema CNOOC iko katika uendelezaji wa miradi ya Benki za Ufukweni
katika Mataifa ya Nigeria, Equitorial Guinea, Congo Brazaville,
Kenya na Uganda.
Akitoa shukrani zake Makamu wa Pili wa Rais wa
Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ameueleza ujumbe huo wa Kampuni ya Kimataifa ya
uwekezaji wa Mafuta na Gesi ya China kwamba Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar imeshajidhatiti katika kutoa ushirikiano wa kina kwa Taasisi au
Kampuni ye yote iliyoonyesha nia ya kutaka kuwekeza miradi yao ya Kiuchumi
Zanzibar.
“
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iko tayari kutoa ushirikiano wa Karibu katika
kuona malengo ya Kampuni ya CNOOC yanafanikiwa vyema “. Alisema Balozi Seif.
Amesema Suala la Mafuta na Gesi kwa sasa
tayari limeshapatiwa maamuzi na Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania
kwa kutolewa ndani ya Mambo ya Muungano ili kuipa fursa pana Zanzibar
kushughulikia yenyewe katika dhana nzima ya kujiimarisha Kiuchumi.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amesema
Zanzibar itaanza matayarisho kamili ya umiliki wa Sekta hiyo pamoja na Kuunda
Shirika litakaloshughulikia Sekta ya Mafuta na Gesi mara baada ya kukamilika
rasmi kipindi cha mpito cha uchaguzi Mkuu wa Zanzibar.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa
Pili wa Rais wa Zanzibar
16/12/2015.
0 comments:
Post a Comment