November 25, 2015

Wakulima wa zao la karafuu kisiwani Pemba, wanahofia kushuka kwa mavuno ya zao hilo kutokana na karafuu kuanza kuanguka kabla ya kipindi cha mavuno.
Hii ni kutokana na karafuu kuzaliwa katika kipindi cha jua na baadae kunyeshewa na mvua  zinazoendelea kabla ya kupevuka.
Wamesema miezi mitatu iliyopita, waliingia na tamaa kuvuna karafuu nyingi msimu huu hasa kutokana na bei kuwa ya juu lakini kwa sasa wanaona matumaini yao hayo yamepotea.
Wakizunguma na mwandishi wa habari hizi kwa nyakati tofauti kisiwani humo wamesema hali hiyo inatishia hasa kwa wale walioamua kukodi karafuu mwezi mmoja uliopita.
Mmoja kati ya wakulima hao Mohamed Haji wa Wambaa Mkoani amesema hasara kwa baadhi ya matajiri waliokodi mashamba ya mikarafuu, imeanza kujitokeza ndani wiki tatu tokea mvua kuanza kunyesha.
Kwa upande wake Hilali Alawi Hija aliekodi shamba la karafuu eneo njia Gando Wete amesema hasumbuliwi na tatizo la wizi lakini amepata mshituko baada ya kugundua kuanguka karafuu kwa wingi.
Hata hivyo amesema iwapo zitasita kuanguka ana matumaini huenda wakarejesha angalau fedha zao walizokodia kwa vile zimeanza kupevuka.
Hata hivyo Mdhamini wa Shirika la Taifa la Biashara Zanzibar ZSTC, Pemba Abdalla Ali Ussi amesema hali hiyo ni ya kawaida kujitokeza kama karafuu zitaanza kuzaliwa kwenye msimu wa jua na kisha kupata mvua.
“ Hili lisiwashituwe sana wakulima na matajiri, maana kuanguka huko kwa karafuu matokeo yake kwa zile zilizobakia huwa na ubora wa hali juu karibu mara mbili” amesema.
Katika hatua nyengine  amesema matarajio kwa mwaka huu kwa Zanzibar ni kununua tani 3200 za karafuu na tayari tani 580 zimeshanunuliwa lakini kwa mwaka jana matarajio hayajafikiwa na walinunua tani zisizodizi 250 kati ya tani 895 walizokisia.

 Haji Nassor, Pemba

0 comments:

Post a Comment