Wanahabari wanapaswa kuwa makini zaidi katika utoaji wa
Habari zao hasa kipindi hichi ambacho Zanzibar inaendelea
kutafuta njia muwafaka ya hatma yake ya baadaye kufuatia Tume ya Uchaguzi
ya Zanzibar { ZEC } kufuta Uchaguzi Mkuu wa Mwezi Oktoba mwaka huu baada
ya kubaini hitilafu kadhaa katika zoezi zima la uchaguzi.
Nasaha hizo zimetolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa
Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi hapo Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar
alipotoa ufafanuzi wa kina juu ya taarifa zilizotolewa na baadhi ya
vyombo vya Habari vikieleza kuwa Viongozi wanaokutana kujadili suala hilo
wamekubaliana kurudiwa kwa uchaguzi huo.
Alisema Kalamu za waandishi wa Habari kwa sasa ni vyema
zikawaelekeza na kuwaongoza Wananchi kujihusisha na harakati zao za kimaisha
badala ya kuwaendeleza katika wimbi la mizozano na mifarakano inayoweza
kuamsha hamasa.
Balozi Seif akiongea na Redio ya Kiswahili ya Kimataifa ya
Ufaransa { RFI } juzi alichokisema kuwaeleza wanahabari hao ni kwamba Chama cha
Mapinduzi {CCM} pekee ndicho kilichotamka na kuthibitisha kuwa kiko tayari
kurejea uchaguzi huo endapo utapangwa upya.
“ Nilichokieleza juzi ni kwamba CCM peeke ndio
Tuliothibitisha na kukubali kurejea uchaguzi endepo utapangwa tena na
hili tunaloendelea nalo la vikao na wenzetu bado tunajadiliana na maamuzi ya
pamoja yatatolewa kwa Waandishi hapo baadaye “. Alisema Balozi Seif.
Alisema hadi sasa hakuna chombo chochote cha Habari ndani
na nje ya Nchi kilichoitwa au kupewa Habari za mazungumzo yanayoendelea
kati ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dr. Ali Mohammed
Shein na Katibu Mkuu wa CUF ambae pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa
Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamadi kwa kuwashirikisha Marais
wastaafu wa Zanzibar.
Balozi Seif alisema utaratibu maalum utaandaliwa wa kutolewa
taarifa rasmi kwa vyombo vyote vya Habari ili ziwafikie Wananchi wote mara
baada ya kukamilika kwa mazungumzo hayo na makubaliano yatakayofikiwa
baina ya pande hizo mbili.
Aliwathibitishia Wananchi na wageni kwamba hali ya Zanzibar bado
iko shwari na salama na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na ile ya
Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia vyombo vyake vya Dola vitasiamia
ipasavyo hali hiyo.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwaomba Wananchi wabakie
kuwa watulivu, wastahamilivu na kuendeleza Umoja na mshikamano
utakaosaidia kulivua Taifa hili katika shari inayoweza kuepukwa.
0 comments:
Post a Comment