November 26, 2015


Jumla ya wagonjwa 226 wa kipindupindu wameripotiwa na kati ya hao watatu wamefariki tangu ulipobainika ugonjwa huo mwezi sept mwaka huu katika shehia mbali mbali kisiwani Unguja.
Idadi hiyo inaelezewa kuengezeka kutokana na wagonjwa wapya kuendelea kupokelewa na kupatiwa matibabu katika kambi ya wagonjwa hao huko chumbuni nje kidogo ya mji wa Zanzibar.
Daktari dhamana wa kituo hicho Ramadhan Mikidadi Suleiman amesema   maeneo yaliyoathirika zaidi ni shehia Kinuni, Fuoni, Shaurimoyo na Kilimahewa.
Akitoa maelezo kwa Mkuu wa mkoa wa mjini Magharib Abdallah Mwinyi Khamis alipotembelea katika kambi hiyo daktari Mikidadi maeneo hayo yameathirika zaidi kutokana na wananchi kuendelea kupuuza maelekezo ya wataalamu wa afya yakiwemo kuchemsha maji ya kunywa na kufanya usafi wa mazingira wa maeneo yao.
Ameeleza kuwa jitihada mbali mbali zimechukuliwa ikiwemo kutoa elimu ya afya kwa wananchi kupiga dawa kwenye maeneo yaliyoathirika na kipindupindu pamoja na kutoa dawa za kulia vidudu katika maji (water guard) kwa familia zilizoathirika na maradhi hayo.
Hata hivyo amefahamisha kuwa kuna baadhi ya wananchi waliopatiwa  dawa hizo wanazitumia kwa kufulia badala ya kutia kwenye maji ya kunywa kama ilivyokusudiwa.

0 comments:

Post a Comment