April 24, 2016

Viongozi wa majimbo pamoja na watu wengine wenye uwezo, wamehimizwa kuendelea kuwasaidia wananchi walioathirika na mvua za masika zinazoendelea kunyesha kote nchini.
Mwakilishi wa jimbo la Tunguu Simai Mohammed Said, amesema maafa yaliyowakumba wananchi mbalimbali, yanahitaji msaada wa kila mwenye uwezo bila kuangalia tofauti za kisiasa, kidini au maeneo waliko.
Said alisema hayo huko Kibele Kwa Bohora, jimbo la Tunguu baada ya kukabidhi mabati 24 yenye thamani ya shilingi laki tatu kwa familia ya mzee Ali Nyau Mavangu na Bi. Tamasina Thomas, ambao nyumba yao ilianguka kutokana na mvua zinazoendelea.
Mwakilishi huyo alisema, kipindi hichi ambacho wananchi wengi wameathiriwa na mvua, ndicho muafaka kwa viongozi wa majimbo walioshinda uchaguzi, kufanya mrejesho kwa wapiga kura wao.
Hata hivyo, alisema jambo la kutoa msaada halipaswi kufanywa na viongozi hao wa majimbo pekee, bali ni wajibu wa kila mmoja kwa uwezo alionao.
Alifahamisha kuwa baada ya kupata taarifa za familia hiyo yenye watoto kadhaa kuangukiwa na nyumba yao usiku wa Aprili 16, mwaka huu, yeye na mbunge wa jimbo hilo Khalifa Salum pamoja na madiwani, wameamua kutoa mabati hayo kuifuta machozi familia hiyo.
Mbali na mabati hayo, pia ameahidi kutoa msaada mwengine wa madirisha na kifusi kwa wananchi hao ambao sasa wanapata usumbufu wa pahala pa kulala kwa amani kutokana na mvua zinazonyesha.
Wakitoa shukurani zao, baba wa familia hiyo mzee Ali Nyau na mkewe Tamasina Thomas, walisema msaada huo umewapa faraja kwani utawawezesha kupata sehemu nzuri ya kujistiri.
Walieleza kufurahishwa sana na viongozi wao kwa hatua ya haraka waliyochukua kuwasaidia, mara baada ya kupata taarifa za maafa yaliyowapata.
“Hatuna neno linaloweza kutosha kuelezea shukurani zetu, lakini kubwa ni kuwaombea dua viongozi wetu hawa Mwenyezi Mungu awazidishie moyo wa imani na waendelee kuwa pamoja nasi katika shida na raha,” walisema.

Aidha, walisema kufuatia kupata msaada huo, wametambua kwamba kura zao hazikupotea na zimekwenda kwa watu sahihi.

0 comments:

Post a Comment