Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza
la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein amesema dhamira ya Serikali ni kuona
watumishi wake wanapata maslahi mazuri zaidi ili kumudu gharama za maisha.
Pamoja na dhamira hiyo, hata hivyo, utekelezaji
wake utategemea zaidi ukuaji wa uchumi ambao utatoa mapato zaidi kwa ajili ya
kugharimia uendeshaji wa shughuli za serikali ikiwemo mishahara, alisema Dk.
Shein.
Akizungumza na ujumbe wa viongozi wa
Shirikisho la Vyama Huru vya Wafanyakazi Zanzibar (ZATUC) ofisini kwake Ikulu
jana, Dk. Shein alisema viongozi wa wafanyakazi wanapaswa kuelewa hali halisi
ya mapato ya serikali na ugumu unaoambatana na kuongeza maslahi ya watumishi
bila kuzingatia mapato halisi ya serikali.
“Sisi (serikali) wafanyakazi wametuchagua
kuwaongoza na nyinyi (viongozi wa ZATUC) ni hivyo hivyo wamewachagua
kuwawakilisha. Kwa hivyo ni viongozi kama sisi; hivyo wajibu wetu ni mmoja tu
kuwatumikia wafanyakazi,” Dk. Shein alisema.
Rais Shein alitoa wito kwa viongozi wa ZATUC
kuendelea na mashauriano na serikali mara kwa mara ili kuzitafutia ufumbuzi
changamoto mbalimbali zinazowakabili wafanyakazi nchini na kuwapa taarifa mara
kwa mara wafanyakazi juu ya hatua zinazofikiwa.
“Milango iko wazi, tuendelee kushauriana mara
kwa mara isiwe karibu na ‘Mei Day’ tu," alisema Dk. Shein.
"Wote lengo letu ni moja ambalo
ni kuwatumikia wafanyakazi wenzetu.”
Aliutaka uongozi wa ZATUC kuendelea kufanya
kazi kwa karibu na serikali na kufuatilia hatua kwa hatua utekelezaji wa
makubaliano mbalimbali yanayofikiwa wakati wa vikao vya mashauriano kati ya
serikali na vyama vya wafanyakazi.
Dk. Shein aliongeza kuwa katika kipindi cha
miaka mitano iliyopita serikali imechukua hatua mbalimbali za kuimarisha
maslahi ya watumishi wa umma na kuahidi kuendelea kufanya kila jitihada kulipa
malimbikizo ya madeni ya watumishi, ikiwemo malipo ya likizo.
Katika mazungumzo hayo ZATUC lilimpongeza Dk.
Shein na serikali yake kwa kuimarisha maslahi ya watumishi na kuongeza fursa za
ajira nchini.
“Tunazipongeza jitihada zako na za serikali
unayoingoza kwa kuimarisha muundo wa utumishi wa umma na maslahi ya watumishi
pamoja na kuongeza ajira nchini” Katibu Mkuu wa ZATUC, Khamis Mwinyi
Mohamed alisema.
Alibainisha kuwa ZATUC imefurahishwa sana na
ahadi ya Mheshimiwa Rais ya kuongeza mshahara wa kima cha chini hadi kufikia
Sh. 300,000.00 kwa mwezi.
“Tunashukuru kuona kati ya mambo 12
tuliyozungumza katika kikao chetu cha tarehe 14 Aprili mwaka jana, mambo 10
yametekelezwa au yamo katika utekelezaji,” alisema Katibu Mkuu
huyo.
0 comments:
Post a Comment